Jumatatu, 13 Machi 2017

SHIRK NA TAWHID

1.1.                     Shirk.
·         Maana : Shirk ni kinyume cha Upweke au Umoja (Tawhiid)
·         Maana ya Kumshirikisha Mwenyezi Mungu (s.w):
Ni kujaalia kinadharia au kiutendaji kuwa kuna miungu wengine wanaoshirikiana na Mwenyezi Mungu (s.w) katika kuongoza na kuendesha Ulimwengu.

§  Aina za Shirk.
Kuna aina kuu nne za shirk,
1.      Shirk katika Dhati ya Mwenyezi Mungu – (Shirk fiy Dhaat).
2.      Shirk katika Sifa za Mwenyezi Mungu – (Shirk fiy Sifaat).
3.      Shirk katika Mamlaka ya Mwenyezi Mungu – (Shirk fiy Ikhtiyaar).
4.      Shirk katika Hukumu za Mwenyezi Mungu – (Shirk fiy Ah-kaam).
                                                                                                                  
        1. Shirk katika Dhati ya Mwenyezi Mungu (s.w).
Ni kujaalia au kuvinasibisha viumbe na uungu kwa kuvipa majina rasmi kama washirika wa Mwenyezi Mungu (s.w) na kuviendea kwa unyenyekevu na ibada maalum kama, kuvisujudia, kuchinja na kuviomba msaada.
Rejea Qur’an (25:2-3), (22:73) na (29:41).

                 2.  Shirk katika Sifa za Mwenyezi Mungu (s.w).
Ni kuwasifu au kuwatukuza viumbe kiwango anachostahiki kusifiwa au kutukuzwa Allah (s.w) peke yake. Kama kuomba dua, baraka na msaada kupitia kwa Wacha-Mungu, mfano kwa baraka za Mtume, Abdul-Qadir, Sharifu au Sheikh fulani n.k.
Rejea Qur’an (53:32), (10:62-64), (2:180), (17:110) na (40:60).

                  3.  Shirk katika Mamlaka ya Mwenyezi Mungu (s.w).
Ni kuwakabidhi viumbe mamlaka kamili ya Mwenyezi Mungu (s.w) na kuwatii kwayo kama vile kuongoza, kulisha, kulea, kulinda n.k katika maisha ya kila siku kinyume na nafasi au uwezo wao.
Rejea Qur’an (9:31) na (2:208).

                  4. Shirk katika Hukumu za Mwenyezi Mungu (s.w).
Ni kutunga sheria au hukumu kinyume na sheria au hukumu za Mwenyezi Mungu (s.w) alizoziainisha katika vitabu vyake vitukufu na kuzitumia kuhukumu kwazo katika uendeshaji wa maisha ya kila siku.
Rejea Qur’an (5:38), (24:2), (33:36), (5:44-45, 47) na (5:50).


§  Kina cha Uovu wa Shirk.
o   Ni dhulma kubwa kuliko zote na ndio chanzo cha matatizo yote ulimwenguni.
Rejea Qur’an (31:13) na (10:35-36).
o   Ni dhambi kubwa kuliko zote isiyosameheka ila apende Mwenyezi Mungu (s.w) na kutubia kikweli kweli kabla ya kufa.
o   Ni dhambi inayofuta mema yote ya mtu aliyoyafanya kabla ya kushirikisha.
Rejea Qur’an (4:48), (4:116) na (39:65).

§  Maana ya Kumuamini Mwenyezi (s.w) katika maisha ya kila siku.
Ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu (s.w) kwa kufuata barabara mwongozo wake katika utendaji wa wetu wa kila kipengele cha maisha yetu ya kila siku kwa kufanya moja kati ya mambo yafuatayo;
o   Kusimamisha Tawhiid (Umoja na Upweke wa Mwenyezi Mungu) na
o   Kujiepusha na Shirk za aina zote.


§   Tawhiid.
o   Kimaana:  Ni Umoja au Upweke wa Mwenyezi Mungu (s.w).
o   Kimatumizi:   Ni fikra, mtazamo wa kimapinduzi katika kumkomboa
mwanaadamu na aina zote za utumwa wa kibinaadamu na kuwa   mtumishi huru wa Muumba wake. 


§  Aina za Tawhiid.
Kuna aina kuu tatu za Tawhiid kama zilivyoainishwa katika aya za Qur’an.

(i)  Tawhid Al-Uluuhiyyah – Upweke wa Allah (s.w) katika Uungu wake.
Nayo ni Kumpwekesha Mwenyezi Mungu (s.w) katika Uungu wake kwa kutokuwa na mungu mwingine yeyote wa kumuelekea kwa ibada au maombi isipokuwa yeye peke yake.
Rejea Qur’an (2:163), (3:62) na (112:1-4).

   (ii)  Tawhiid Al-Asmaa Wassifaat – Upweke wa Mwenyezi Mungu (s.w) katika Majina     
                                                                 na Sifa.
Nayo ni kutomsifu Mwenyezi Mungu (s.w) kwa sifa za viumbe au majina ya viumbe na pia kutomsifu kiumbe yeyote kwa sifa za Mwenyezi Mungu (s.w).
Rejea Qur’an (57:1-6) na (59:22-24).

 (iii) Tawhiid Rabbuubiyya – Upweke wa Mwenyezi Mungu (s.w) katika Ubwana,Utawala
                                                   na Mamlaka Yake. 
Kumpwekesha Allah (s.w) katika Ubwana na Utawala wake ni kutofuata na sheria na taratibu za maisha kinyume na zile alizoziweka yeye kwa kumfanya ndiye Mlezi, Mlinzi, Mwendeshaji wa kila kitu.
Rejea Qur’an (4:59), (31:14-15), (25:52), (3:149), (3:100) na (5:57).