Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu michezo inayokubalika
katika dini na ile isiyokubalika.
Hakuna uharamu wowote kwa mtu kucheza mchezo wowote ule ambao unakwenda
sambamba na shari’ah, kuangalia au kuwa shabiki kwa mipaka ya Uislamu.
Tufahamu kuwa Uislamu ni Dini ya vitendo wala sio ya nadharia.
Inawachukulia wanaadamu kama wanaadamu. Kwa ajili hiyo, Uislamu ni Dini na
dunia. Kuna namna nyingi ya michezo waliowekewa Waislamu na Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili kujifurahisha na kujipumzisha, nayo
kwa wakati huo yanaitayarisha nafsi zao kuweza kufanya ‘Ibaadah zao na wajibu
wao kwa nashati kubwa zaidi na hima kubwa zaidi. Nyingi katika hizo ni Riyadha
zinazowazoweza kupambana na mazito, na kuwatayarisha kwa vita vya Jihaad na
kupigana kwa ajili ya Allaah Aliyetukuka. Katika michezo iliyo halali ni kama
ifuatayo:
1. Mbio, naye Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anashindana na mkewe ‘Aa’ishah
(Radhiya Allaahu ‘anha).
2. Miereka, naye Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alishindana na Rukaana na
kumshinda (Abu Daawuud na Ahmad).
3. Kurusha mishale. Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwapita Maswahaba (Radhiya
Allaahu ‘anhum) wakishindana kurusha mishale, naye akawahimiza kwa kuwaambia:
“Rusheni nami ni pamoja nanyi” (al-Bukhaariy).
4. Kucheza na mikuki.
5. Kupanda farasi.
6. Kuogelea pia kumehimizwa
sana.
7. Kuwinda kwa kutumia ala
kama mishale, mikuki na kwa sasa bunduki.
Uislamu pia umeweka kanuni za kijumla ya kuufanya mchezo wowote ule
kuwa halali au haramu. Kanuni hizo ni kama zifuatazo:
1. Uhalali unategemea manufaa
au hasara inayopatikana. Ikiwa manufaa ni makubwa zaidi mchezo utakuwa halali
na lau itakuwa kinyume chake basi utakuwa ni haramu.
2. Mchezo wowote wenye kamari
unakuwa ni haramu.
3. Isicheleweshwe Swalah
kutoka kwa wakati wake kwa ajili ya mchezo wowote ule. Hatari hiyo inakuwa
kubwa kwa kupoteza wakati na kujishughulisha watu kukosa kutekeleza wajibu wao.
4. Mchezaji ahifadhi ulimi
wake wakati wa kucheza, asitukane na kutokwa na maneno machafu.
5. Mchezo kama wa ngumi ni
mchezo uliokuwa haufai kwani kuna kudhuriuana uso ambako kumekatazwa na Mtume
wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuleta madhara ya ubongo
na mifano ni mingi.
6. Mavazi yalingane na stara
ya iliyowekwa kishari’ah. Haifai kuvaa vikaptula vinavyonyesha mapaja ya
mwanaume kama ilivyo kwenye mpira wa miguu na mbio na pia nguo za kubana zenye
kuonyesha maungo ya ndani kama kwenye michezo ya kukimbia, kuogelea, michezo ya
viungo kama jimnastiki (sarakasi) n.k.
7. Wanawake hawakatazwi
kucheza maadam wako wenyewe, na wawe wamevaa stara za kishari’ah. Hata hivyo
wanawake haiwapendezei kucheza michezo ya nguvu iliyo kinyume na maumbile yao
kama mieleka, mpira wa miguu na mingine ambao wanawake wa siku hizi wameanza
kuiga.
Ikiwa moja katika masharti yaliyo juu haikutimizwa, basi mchezo huo
utakuwa ni haramu. Hivyo, uhalali na uharamu kucheza mchezo wowote itagemea na
vigezo vilivyo juu.
Na Allaah Anajua zaidi