Jumapili, 21 Mei 2017

DARSA LA FUNGA

          SAUMU YA FARDHI (Ramadhani)
Nini Saumu?
Saumu kilugha ni kujizuiya na kitu, yaani kutofanya kitu fulani; kama ilivyo kwenye QurĂ¡ni Tukufu:
  " ......... Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu ya kufunga; kwa hivyo leo sitasema na mtu". (Maryam : 26).
Kisharia Saumu ni kujizuia kula, kunywa na matamanio ya utupu; tangu alfajiri mpaka kutua jua pamoja na kutia nia ya hio saumu. Hivi kutia nia ni kwa qauli ya Mtume s.a.w. kwa kukhusu kila ibada, yaani kutimia ibada ni kuwepo na kutimia nia:  Maana ya Hadithi hii ni kama hivi:
"Hakika ya kila kitendo ni kwa nia yake".


              Hukmu Yake
Saumu ni nguzo ya nne kati ya nguzo tano za Uislam. Kulazimika saumu kumekuja kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kufasiriwa kwa qauli ya Mtume s.a.w. na wanazuoni wakawafiqiana juu ya hili. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyo andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuchamngu”. (Al Baqara : 183).
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:
   "..... Basi ataye kuwa mjini katika mwezi huu naafunge.....".(Al Baqara : 185).
Na Hadithi ya Mtume s.a.w.:   Maana ya Hadithi hii ni kama hivi: "Umejengwa Uislam juu ya (Nguzo) tano".
Katika nguzo tano hizo, ikatajwa nguzo ya nne kuwa ni Saumu ya mwezi wa Ramadhani. Mtu alimuomba Mtume s.a.w. amfahamishe saumu alioifaridhisha Mwenyezi Mungu Mtukufu juu yake. Akasema Mtume s.a.w.:  , yaani Saumu ya Mwezi wa Ramadhani".
Saumu imewajibikishwa juu ya Muislam, baalegh, mwenye akili kaamili, mwenye uwezo wa kufunga. Saumu haimuwajibikii Kafiri wa asili, wala haisihi juu yake Saumu, kwa vile yeye si mwenye kuhisabika kuwa ni katika wenye kufanya ibada, vilevile Saumu haimuwajibikii mtoto mdogo. Saumu haimlazimikii mtoto, lakini mtoto huzoeleshwa kufunga tangu udogoni. Vilevile Saumu haimuwajibikii mgonjwa wa akili. Hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:

Maana ya Hadithi hii ni kama hivi:
"Imeondoshwa kalamu (kulazimika na hukmu za Sharia) kwa watu watatu: mwenye kulala mpaka aamke, mtoto mdogo mpaka abaleghe, na mgonjwa wa akili mpaka apowe". (Imehadithiwa na Abu Daud).
Ama yule asieweza kufunga, au kama atafunga atapata madhara ambayo hayatarajiwi, hivi ni kama vile mtumzima (mkubwa wa umri), au mtu mwenye maradhi ambayo hayatarajiwi kupona, hawa haiwajibikii juu yao kufunga, lakini itawalazimikia kafara. Kafara ya katika hali hii ni kutoa kibaba cha chakula cha kawaida cha nchini kwa kila siku
anayoshindwa kufunga, ikiwa ni mwenye uwezo wa kufanya hivyo, ikiwa
hana uwezo, baadae akapata uwezo itamlazim atekeleze kafara hii ambayo ni dhima juu yake.

           Fardhi za Saumu
Saumu ina fardhi tano:
Ya Kwanza, nia; na mahala pake ni moyoni; na ni waajibu kutia nia kila usiku wa kuamkia (kabla ya alfajiri) siku ya saumu. Hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:    "Asietia nia (ya kufunga, Saumu ya fardhi) tangu kabla ya alfajiri basi hana Saumu". (Imehadithiwa na Ahmad na wapokezi wa Hadithi).
Ya Pili na Tatu, kujizuia kula na/au kunywa hata chembe ndogo tangu kuingia alfajiri mpaka kuingia magharibi. Kujizuia huku ni kwa kujizuia na kila kitu kufika tumboni/ndani ya mwili kwa njia ya tundu za mwili zilizo wazi, kujizuia huku kuwe kunakusudiwa khaasa kwa ajili ya kutekeleza hii ibada ya saumu.
Ya Nne, kujizuia kuingilia utupu wowote ule na/au kujitoa manii kwa njia yoyote ile, ikiwa kwa mkono au kwa kuchezeana. Haya ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
"
.…..Basi sasa changanyikeni nao na takeni aliyo kuandikieni Mwenyezi Mungu. Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Saumu mpaka usiku.........". (Al Baqara : 187).
Ikiwa mtu atatokezea akala au akanywa hali ya kuwa amesahau kuwa ana saumu; Saumu yake haitaba'tilika; hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:
 "Mwenye kusahau kuwa kafunga, akala au akanywa; basi naatimize Saumu yake kwani yeye amelishwa na amenywishwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu". (Imehadithiwa na Jama'a Wapokezi Hadithi)
Vilevile kwa qauli ya Mtume s.a.w.:
 "Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu amewasamehe umati wangu kwa la kukosea na la kusahau na la kulazimishwa". (Imehadithiwa na Ibnu Maajah na Al 'Tabrany na Al Haakim).
Ya Tano, kujizuia na kujitapisha. Ikiwa atatapika bila ya kukusudia basi Saumu yake haitaba'tilika, hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:
   "Mwenye kutapika (si makusudi) nae amefunga, haimlazim kuilipa Saumu yake, na mwenye kujitapisha (makusudi) basi naailipe Saumu yake". (Imehadithiwa na Wapokezi Hadithi).

            MAREJEO