Alhamisi, 27 Septemba 2018

Namna ya kuswali: 1. Nia



Mtume (s.a.w) ametuagiza katika Hadith maarufu kuwa tuswali kama alivyokuwa akiswali. Hivyo katika sehemu hii tutajitahidi kuonesha utekelezaji wa swala hatua kwa hatua kwa kurejea Hadith Sahihi za Mtume (s.a.w):

1. Nia na Takbira ya kuhirimia
 Nia ni kudhamiria moyoni kuwa unaswali, swala unayoikusudia kisha unaanza swala kwa kusema: “Allaahu Akbar” Allah ni Mkubwa kwa kila hali”. Wakati wa kuhirimia swala ni sunnah kuinua viganja vya mikono,mkabala na mabega. Kuhusu unyanyuaji wa mikono mkabala na mabega imeripotiwa kuwa Mtume (s.a.w) alikuwa akifanya hivyo katika sehemu nne tofauti:
 1. Wakati wa kuhirimia swala (kuanza swala).


2. Wakati anaposema Allaahu Akbar kwa ajili ya rukui.

3. Wakati anaposimama kutoka kwenye rukuu.

4. Wakati anaposimama kutoka kwenye tahiyyatu ya kwanza ili kuendelea na rakaa ya tatu.

 Hii tunaipata katika Hadith aliyosimulia Abdullah bin ‘Umar kuwa: “Mtume (s.a.w) aliposimama kwa ajili ya swala alinyanyua mikono yake mkabala na mabega yake na kisha kuhirimia (kusema Allahu Akbar). Alipotaka kurukuu alinyanyua mikono kama alivyofanya kwanza na aliposimama kwa ajili ya itidali alifanya hivyo hivyo na alisema Allah anamsikia yule anayemsifu. (Bukhari, Muslim na Bayhaqi).
Nafa’a(r.a) ameeleza kwamba Ibn ‘Umar (Abdullah)(r.a) aliposimama kwa ajili ya rakaa ya tatu alikuwa akinyanyua mikono; jambo ambalo alilihusisha na Mtume (s.a.w). (Bukhari, Abu Dawud, Nasai).

 Baada ya kuhirimia swala mwenye kuswali hushusha mikono yake na kuiweka kifuani, mkono wa kulia ukiwa juu ya mkono wa kushoto kwa mujibu wa Hadith zifuatazo: Hulab At-Tai(r.a) amesimulia: “Nilimuona Mtume (s.a.w) akiswali hali ameweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto juu ya kifua chake.” (Ahmad na At-Tirmidh)

Naye Wail bin Hijr (r.a) ameripoti: “Niliswali pamoja na Mtume (s.a.w) na aliweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto juu ya kifua chake”. (Ahmad na At-Tirmidh).

Imamu Abu Dawud na Nasai wamepokea kutoka kwa Ibn Khuzaimah kuwa Mtume (s.a.w) alipokuwa akiswali alikuwa akiweka mkono wake wa kulia juu ya kiwiko (wrist) cha mkono wa kushoto na sehemu ya mkono inayofuatia kiganja .