Fadhila Za Qiyaamul-Layl
(Kisimamo Cha Kuswali Usiku)
www.alhidaaya.com
Uaweza kupata darsa nyingi za dini ukiwa na program zetu mbali mbali bofya hapa.
kupata dua mbali mbali bofya hapa
Elimu ya Afya na vyakula bofya hapa
Elimu ya lishe bofya hapa
Muislamu anapaswa asikose Qiyaamul-Layl khasa katika mwezi wa Ramadhwaan kwa sababu ya Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((مَنْ قَامَ رَمَضَانَ إِيمَانًا وَاحْتِسَابًا غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ))
رواه البخاري 37 ومسلم 759
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayesimama kuswali Ramadhwaan kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Al-Haafidh Ibn Rajab (Rahimahu Allaah) amesema: "Tambua kuwa Muumini anajumuisha katika mwezi wa Ramadhwaan jihaad mbili kwa ajili ya nafsi yake; jihaad ya mchana ya kufunga, na jihaad ya usiku kwa kusimama (kuswali), atakayejumuisha jihaad hizi mbili atapata ujira wake bila ya hesabu".
Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema: "Haimpasi Muislamu kuepukana na Swalaah ya Tarawiyh katika Ramadhwaan ili apate thawabu na ujira wake, na wala asiondoke mpaka Imaam amalize Swalaah ya Witr ili apate ujira kamili wa Qiyaamul-Layl".
Ili kuipata ladha ya Ramadhwaan na kuongeza utiifu, ni muhimu Muislamu ajumuike na Waislamu wenzie kuswali Tarawiyh asikilize Qur-aan inaposomwa katika Swalaah hizi kwa sababu itampatia utulivu wa moyo na pia atajichumia thawabu adhimu zinazopatikana katika kisimamo hiki kinachofuta madhambi kama ilivyotajwa katika Hadiyth iliyotangulia.
Fadhila Za Qiyaamul-Layl:
1-Qiyaamul-Layl ilikuwa ni amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Waumini wakatekeleza:
يَا أَيُّهَا الْمُزَّمِّلُ﴿١
Ee uliyejifunika.
قُمِ اللَّيْلَ إِلَّا قَلِيلًا﴿٢
Simama (kuswali) usiku kucha isipokuwa kidogo tu.
نِّصْفَهُ أَوِ انقُصْ مِنْهُ قَلِيلًا﴿٣
Nusu yake, au ipunguze kidogo.
أَوْ زِدْ عَلَيْهِ وَرَتِّلِ الْقُرْآنَ تَرْتِيلًا﴿٤
Au izidishe, na soma Qur-aan kwa kisomo cha utaratibu upasao, kuitamka vizuri na kutaamali. [Al-Muzzammil 1-4]
Na pia Amemuamrisha tena Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
أَقِمِ الصَّلَاةَ لِدُلُوكِ الشَّمْسِ إِلَىٰ غَسَقِ اللَّيْلِ وَقُرْآنَ الْفَجْرِ ۖ إِنَّ قُرْآنَ الْفَجْرِ كَانَ مَشْهُودًا ﴿٧٨
Simamisha Swalaah tokea kupinduka hadi kukuchwa jua mpaka kiza cha usiku na Qur-aan ya (Swalaah ya) Alfajiri. Hakika Qur-aan ya Alfajiri ni yenye kushuhudiwa.
وَمِنَ اللَّيْلِ فَتَهَجَّدْ بِهِ نَافِلَةً لَّكَ عَسَىٰ أَن يَبْعَثَكَ رَبُّكَ مَقَامًا مَّحْمُودًا ﴿٧٩
Na katika usiku, amka uswali nayo (tahajjud) ni ziada ya Sunnah kwako. Asaa Rabb wako Akakuinua cheo kinachosifika. [Al-Israa: 78-79]
Mujaahid amesema: "Qiyaam kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni naafilah (Sunnah ya ziada) kwa sababu ameshafutiwa madhambi yake yaliotangulia na ya mbele. Na kwa Ummah wa Kiislamu, Swalaah ya Qiyaamul-Layl huenda pia ikamfutia mtu madhambi yake atakayotenda". [Atw-Twabariy 17:525]
Anasema tena Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
فَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ الْغُرُوبِ﴿٣٩
Subiri juu ya yale wanayoyasema, na sabbih kwa Himidi za Rabb wako kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa.
وَمِنَ اللَّيْلِ فَسَبِّحْهُ وَأَدْبَارَ السُّجُودِ﴿٤٠
Na katika usiku Msabbih na baada ya kusujudu. [Qaaf: 39-40]
Na:
وَاذْكُرِ اسْمَ رَبِّكَ بُكْرَةً وَأَصِيلًا﴿٢٥
Na lidhukuru Jina la Rabb wako asubuhi na jioni.
وَمِنَ اللَّيْلِ فَاسْجُدْ لَهُ وَسَبِّحْهُ لَيْلًا طَوِيلًا﴿٢٦
Na katika usiku msujudie na uswali kwa ajili Yake usiku mrefu. [Al-Insaan: 25-26]
2-Qiyaamul-Layl ni njia mojawapo ya kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa
Kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) sio kwa kutamka tu bali kwa kukiri moyoni na kwa matendo. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisimama usiku kuswali mpaka miguu yake ilikuwa ikivimba:
عَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا: أَنَّ نَبِيَّ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ كَانَ يَقُومُ مِنَ اللَّيْلِ حَتَّى تَتَفَطَّرَ قَدَمَاهُ، فَقَالَتْ عَائِشَةُ: لِمَ تَصْنَعُ هَذَا يَا رَسُولَ اللَّهِ، وَقَدْ غَفَرَ اللَّهُ لَكَ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِكَ وَمَا تَأَخَّرَ؟ قَالَ: ((أَفَلاَ أُحِبُّ أَنْ أَكُونَ عَبْدًا شَكُورًا)) متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisimama usiku hadi ikivimba miguu yake, nikamwambia: “Kwa nini unafanya hivi ee Rasuli wa Allaah na hali umefutiwa madhambi yako yaliyotangulia na yatakayofuatia?” Akasema: ((Je, nisiwe mja mwenye kushukuru?)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
3-Qiyaamul-Layl ni Swalaah bora kabisa baada ya Swalaah ya fardhi kwa kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((أَفْضَلُ الصَّلاةِ بَعْدَ الْفَرِيضَةِ صَلاةُ اللَّيْلِ)) رواه مسلم.
((Swalaah iliyo bora kabisa baada ya fardhi ni Swalaah ya usiku)) [Muslim]
4-Qiyaamul-Layl ni kufuata na kufufua Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na pia Qiyaamul-Layl ilikuwa ni desturi ya Salaf na sababu kuu ya kumzidishia Muislamu iymaan yake na kumtakasa moyo kutokana na maovu mengi; uasi, unafiki, chuki, uhasidi n.k. Pia nyoyo hupata utulivu na huelekea kwa yanayomridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((عليكُم بقيامِ اللَّيلِ ، فإنَّهُ دَأْبُ الصَّالِحينَ قبلَكُم ، و قُربةٌ إلى اللهِ تعالى ومَنهاةٌ عن الإثمِ و تَكفيرٌ للسِّيِّئاتِ ...))
((Shikamaneni na Qiyaamul-Layl (kuswali usiku) kwani ni desturi za waja wema kabla yenu, na kujikurubisha kwa Allaah Ta’aalaa, na inazuia madhambi, inafuta maovu…)) [Ahmad na At-Tirmidhiy na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami (4079)]
‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa akipitia usiku akisikia kisomo cha Qiyaamul-Layl, akazimia siku moja yakapita masiku akiugua hadi akapona [Munswaf Ibn Abiy Shaybah]
Na yamemthibiti mengi kuhusiana na hali za Salaf kusimama kwao usiku kuswali.
bofya
5-Qiyaamul-Layl ni kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
عن عَمْرُو بْنُ عَبَسَةَ، أَنَّهُ سَمِعَ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، يَقُولُ: ((أَقْرَبُ مَا يَكُونُ الرَّبُّ مِنَ العَبْدِ فِي جَوْفِ اللَّيْلِ الآخِرِ، فَإِنْ اسْتَطَعْتَ أَنْ تَكُونَ مِمَّنْ يَذْكُرُ اللَّهَ فِي تِلْكَ السَّاعَةِ فَكُنْ)) الترمذي هَذَا حَدِيثٌ حَسَنٌ صَحِيحٌ
Imepokelewa kutoka kwa 'Amru bin 'Abasah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba kamsikia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Wakati Allaah Anakuwa karibu kabisa na mja, ni wakati wa mwisho wa usiku, kwa hiyo ukiweza kuwa miongoni mwa wanaomdhukuru Allaah katika saa hiyo basi uwe)) [At-Tirmidhy ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy (3579), Swahiyh Al-Jaami’ (1173)]
6-Qiyaamul-Layl ni kujikinga na maovu ya shaytwaan:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بن مسعود رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ، قَالَ: ذُكِرَ عِنْدَ النَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ رَجُلٌ، فَقِيلَ: مَا زَالَ نَائِمًا حَتَّى أَصْبَحَ، مَا قَامَ إِلَى الصَّلاَةِ، فَقَالَ: ((ذَاكَ رَجُلٌ بَالَ الشَّيْطَانُ فِي أُذُنِهِ)) روى البخاري (1144) ومسلم (774) والنسائي (1608) وابن حبان (2562)
Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas’-uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba ilitajwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba kuna mtu alilala usiku wote hadi asubuhi bila kuswali, Akasema: ((Huyo ni mtu aliyekojolewa na Shaytwaan katika masikio yake)) [Al-Bukhaariy, Muslim, An-Nasaaiy, Ibn Hibbaan]
‘Ulamaa wamekhitilafiana kusudio la kauli: “mtu alilala usiku wote hadi asubuhi bila kuswali”. Wakataj wengine kuwa ni Swalaah ya fardhi na wengine wakaona ni Qiyaamul-Layl.
7-Wanaoswali Qiyaamul-Layl wameandaliwa Jannah:
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
تَتَجَافَىٰ جُنُوبُهُمْ عَنِ الْمَضَاجِعِ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ خَوْفًا وَطَمَعًا وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿١٦
Mbavu zao zinatengana na vitanda, wanamuomba Rabb wao kwa khofu na matumaini, na katika yale Tuliyowaruzuku wanatoa.
فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٧
Basi nafsi yoyote haijui yaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho. Ni jazaa kwa yale waliyokuwa wakiyatenda. [As-Sajdah: 16-17]
Aayah hizo tukufu zinambashiria Muumini Jannah pindi atakapojitahidi kuamka kuswali usiku pamoja na kutoa mali yake katika njia ya Allaah. Huko Jannah, kuna neema za kufurahisha zenye kudumu milele ambazo hajapatapo mtu kuona wala kusikia wala kuwaza kama ilivyotajwa katika Hadiyth Al-Qudsiy:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ عَنْ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((قَالَ اللَّهُ تَبَارَكَ وَتَعَالَى: أَعْدَدْتُ لِعِبَادِي الصَّالِحِينَ مَا لَا عَيْنٌ رَأَتْ وَلَا أُذُنٌ سَمِعَتْ وَلَا خَطَرَ عَلَى قَلْبِ بَشَرٍ)) قَالَ أَبُو هُرَيْرَةَ اقْرَءُوا إِنْ شِئْتُمْ: (( فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَا أُخْفِيَ لَهُمْ مِنْ قُرَّةِ أَعْيُنٍ)) البخاري، مسلم، الترمذي وابن ماجه
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Tabaaraka wa Ta’aalaa Amesema: Nimewatayarishia waja Wangu wema kile ambacho jicho lolote halijapata kuona na sikio lolote halijapata kusikia na wala haijapata kupita katika moyo wa binaadamu)) Akasema Abuu Hurayrah: Kwa hivyo, soma ukitaka: Basi nafsi yoyote haijui yaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho. Ni jazaa kwa yale waliyokuwa wakiyatenda)) [As-Sajdah: 32:17] [Al-Bukhaariy, Muslim, At-Tirmidhiy na Ibn Maajah]
Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametaja pia kuhusu wanaoamka kuswali usiku:
إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ﴿١٥
Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na chemchemu.
آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَٰلِكَ مُحْسِنِينَ﴿١٦
Wakichukua yale Atakayowapa Rabb wao. Hakika wao walikuwa kabla ya hapo ni wahisani.
كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ﴿١٧
Walikuwa kidogo tu katika usiku wakilala kwa raha. [Adh-Dhaariyaat: 15-19]
Na pia Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
عَنْ عَلِيٍّ قَالَ : قَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : ((إِنَّ فِي الْجَنَّةِ غُرَفًا تُرَى ظُهُورُهَا مِنْ بُطُونِهَا، وَبُطُونُهَا مِنْ ظُهُورِهَا، فَقَامَ أَعْرَابِيٌّ فَقَالَ : لِمَنْ هِيَ يَا رَسُولَ اللَّهِ ؟ قَالَ : ((لِمَنْ أَطَابَ الْكَلامَ وَأَطْعَمَ الطَّعَامَ ، وَأَدَامَ الصِّيَامَ ، وَصَلَّى لِلَّهِ بِاللَّيْلِ وَالنَّاسُ نِيَامٌ )) وحسنه الألباني في صحيح الترمذي .
Imepokelewa kutoka kwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika katika Jannah kuna nyumba ambazo nje yake huonekana ndani na ndani yake huonekana nje)) Bedui mmoja akasimama na kusema: “Ee Rasuli wa Allaah kwa ajili ya nani hizo?”. Akasema: ((Kwa ajili ya wanaotamka maneno mazuri, wanaolisha watu chakula, wenye kudumisha swiyaam, na wenye kuswali usiku wakati watu wengine wamelala)) [At-Tirmidhiy na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy (1984)]
8-Qiyaamul-Layl ni miongoni mwa sifa za waja wa Ar-Rahmaan:
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَعِبَادُ الرَّحْمَـٰنِ الَّذِينَ يَمْشُونَ عَلَى الْأَرْضِ هَوْنًا وَإِذَا خَاطَبَهُمُ الْجَاهِلُونَ قَالُوا سَلَامًا ﴿٦٣
Na waja wa Ar-Rahmaan ni wale wanaotembea katika ardhi kwa unyenyekevu na upole, na majahili wanapowasemesha, wao husema: Salaam!
وَالَّذِينَ يَبِيتُونَ لِرَبِّهِمْ سُجَّدًا وَقِيَامًا ﴿٦٤
Na wale wanaokesha usiku kwa ajili ya Rabb wao wakisujudu na kusimama. [Al-Furqaan: 63-64]
9-Wanaoswali Qiyaamul-Layl si sawa na watu wengine.
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
لَيْسُوا سَوَاءً ۗ مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ أُمَّةٌ قَائِمَةٌ يَتْلُونَ آيَاتِ اللَّـهِ آنَاءَ اللَّيْلِ وَهُمْ يَسْجُدُونَ ﴿١١٣
Hawako sawa sawa; miongoni mwa Ahlil-Kitaabi wako watu wenye kusimama (kwa utiifu) wanasoma Aayaat za Allaah nyakati za usiku na wao wanasujudu (katika Swalaah) [Aal-'Imraan: 113]
Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
أَمَّنْ هُوَ قَانِتٌ آنَاءَ اللَّيْلِ سَاجِدًا وَقَائِمًا يَحْذَرُ الْآخِرَةَ وَيَرْجُو رَحْمَةَ رَبِّهِ ۗ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ ۗ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿٩
Je, yule aliye mtiifu nyakati za usiku akisujudu, au akisimama (kuswali), anatahadhari na Aakhirah na anataraji rahmah ya Rabb wake (ni sawa na aliyekinyume chake?). Sema: “Je, wanalingana sawa wale wanaouja na wale wasiojua?” Hakika wanakumbuka wenye akili tu. [Az-Zumar: 9]
10-Qiyaamul-Layl ni kughufuriwa madhambi.
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa wanaoswali thuluthi ya mwisho ya usiku:
الصَّابِرِينَ وَالصَّادِقِينَ وَالْقَانِتِينَ وَالْمُنفِقِينَ وَالْمُسْتَغْفِرِينَ بِالْأَسْحَارِ﴿١٧
Wenye kusubiri na wasemao kweli, na watiifu, na watoaji mali katika njia ya Allaah na waombao maghfirah kabla ya Alfajiri. [Aal-‘Imraan: 17]
Na katika Hadiyth Al-Qudsiy:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((يَنْزِلُ رَبُّنَا تَبَارَكَ وَتَعَالَى كُلَّ لَيْلَةٍ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا حِينَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الْآخِرُ يَقُولُ: مَنْ يَدْعُونِي فَأَسْتَجِيبَ لَهُ، مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ، مَنْ يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرَ لَهُ)) البخاري و مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Tabaaraka wa Ta’aalaa Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba du’aa Nimuitike? Nani Ananiomba jambo Nimpe? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy, Muslim]
11-Mwenye kuswali Qiyaamul-Layl hujaaliwa siha katika mwili wake.
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amemsema:
((عليكُم بقيامِ اللَّيلِ ، فإنَّهُ دَأْبُ الصَّالِحينَ قبلَكُم ، و قُربةٌ إلى اللهِ تعالى ومَنهاةٌ عن الإثمِ و تَكفيرٌ للسِّيِّئاتِ ، ومَطردةٌ للدَّاءِ عن الجسَدِ))
((Shikamaneni na Qiyaamul-Layl (kuswali usiku) kwani ni desturi za waja wema kabla yenu, na kujikurubisha kwa Allaah Ta’aalaa, na inazuia madhambi, inafuta maovu na inaondosha maradhi mwilini)) [Ahmad na At-Tirmidhiy na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami (4079)]
12-Nyakati za Qiyaamul-Layl ni nyakati za kutakabaliwa du’aa:
عَنْ جَابِرٍ قَالَ : سَمِعْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((إِنَّ فِي اللَّيْلِ لَسَاعَةً لَا يُوَافِقُهَا رَجُلٌ مُسْلِمٌ يَسْأَلُ اللَّهَ خَيْرًا مِنْ أَمْرِ الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ إِلَّا أَعْطَاهُ إِيَّاهُ وَذَلِكَ كُلَّ لَيْلَةٍ)) مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba kamsikia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Hakika katika usiku kuna saa ambayo mja anapomuomba Allaah kheri katika mambo ya dunia au Aakhirah ila (Allaah) Humpa kheri hizo, na hivyo ni kila usiku)) [Muslim]
13-Kuswali Qiyaamul-Layl ni utukufu wa Muumini:
عنْ سهل بن سعد الساعدي عن النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم: ((أتاني جبريلُ ، فقال : يا مُحمَّدُ! عِشْ ما شِئتَ فإنَّك مَيِّتٌ، وأحْبِبْ من شِئتَ فإنَّكَ مُفارِقُه، واعمَل ما شِئتَ فإنَّك مَجْزِيٌّ بهِ، واعلَم أنَّ شرفَ المؤمنِ قيامُه باللَّيلِ، وعِزُّه استِغناؤُه عن النَّاسِ)) رواه الحاكم والبيهقي وحسنه المنذري والألباني
Imepokelewa kutoka kwa Sahl bin Sa’d As-Saa’idiy kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Amenijia Jibriyl akasema: Ee Muhammad ishi upendavyo bila shaka wewe utakuwa maiti, na mpende umtakaye bila shaka utafarikiana naye, na tenda unavyopenda lakini ujue utalipwa kwa vitendo hivyo, na tambua kwamba utukufu wa Muumin ni Qiyaamul-Layl, na heshima yake ni kujitosheleza na watu)) [Hadiyth imepokelewa pia kutoka kwa Jaabir na ‘Aliy Radhwiya Allaahu ‘anhumaa - Al-Haakim na Al-Bayhaqiy, na Al Mundhiriy na Al-Abaaniy wamesema ni Hadiyth Hasan – As-Silsilah Asw-Swahiyhah (831)]
14-Qiyaamul-Layl ni kupata husnul-khaatimah (mwisho mwema)
عبدالله بن عمرو عن النبي صلى الله عليه وسلم ((من قام بعشرِ آياتٍ لم يُكتبْ من الغافلينَ ، ومن قام بمئةِ آيةٍ كُتبَ من القانتينَ ومن قام بألفِ آيةٍ كُتبَ من المُقَنْطِرينَ)) صحيح أبي داود
((Atakayesimama usiku kwa kuswali na kusoma Aayah kumi hatoandikiwa katika miongoni mwa walioghafilika, na atakayesimama kwa Aayah mia ataandikiwa ni miongoni mwa watiifu na atakayesimama kwa Aayah elfu ataandikwa miongoni mwa wenye mirundi [ya thawabu])) [Abuu Daawuwd ameisahihisha Al-Albaaniy: Swahiyh Abiy Daawuwd (1398), Swahiyh Al-Jaami’ (6439)]
15-Nyuso za wanaoswali Qiyaamul-Layl hun’gaa kwa nuru
Hasan Al-Baswriy (Rahimahu Allaah) amesema:
"ما نعلم شيئًا أَشَدَّ من مكابدة اللَّيل ونفقة هذا المال" فقيل : ما بالُ المتهجِّدين من أحسن الناس وجوهًا ؟ قال : "لأنهم خلوا بالرحمن فألبسهم نورًا من نوره" إحياء علوم الدين
"Sijapata kuona ‘ibaadah iliyo nzito kama Swalaah katika kiza cha usiku na kutoa kwake mali". Akaulizwa: “Mbona wale Mutahajjudiyn (wanaoamka usiku kuswali) nyuso zao ni nzuri kabisa?” Akajibu: "Kwa sababu wamejiweka faragha na Ar-Rahmaan, basi Naye Akawavisha Nuru Yake". [Ihyaa ‘Uluwm Ad-Diyn]
Baadhi Ya Yatakayomwezesha Qiyaamul-Layl
1-Kuwa na ikhlaasw katika ‘amali.
2-Kutafakari Hadiyth ya Al-Qudsiy kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anateremka thuluthi ya mwisho kuwakidhia Waislamu haja zao. Nani asiyekuwa na haja, nani asiyekuwa na madhambi ya kughufuriwa? Asiyejihimiza kuamka usiku ni kama kwamba hamhitaji Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amtakakbalie haja zake na Amghufurie dhambi zake!
3-Kutambua fadhila za Qiyaamul-Layl.
4-Kulala katika twahaarah, yaani kutia wudhuu kabla ya kulala.
5-Kusoma nyiradi za usiku na kumuomba sana Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) tawfiyq ya kuamka usiku.
6-Kulala mapema
7-Kutokula sana mpaka mtu akashiba mno.
8-Kutokujitaabisha sana mchana khasa kwa mambo ya kidunia.
9-Usiache 'Qaylulah' (kulala kidogo mchana) kwa sababu ni Sunnah na inamsaidia mtu kumpa nguvu za kuamka usiku.
10-Kutokutenda maasi kwani yanamzuia mtu kutotimiza ‘ibaadah vizuri.
11-Kuutakasa moyo kutokana na maradhi ya moyo; uhasidi, chuki, uadui, ghiybah (kusengenya), an-namiymah (kufitinisha) na kila maovu.
12-Kutafakari mauti na kutokuwa na matumaini ya umri mrefu.