Kukusanywa na Kuhifadhiwa kwa Qur’an.
§ Qur’an
ina ahadi ya kuhifadhiwa na kulindwa na Mwenyezi Mungu (s.w) tofauti na vitabu
vingine kama aya zifuatazo zinavyobainisha;
“Hakika Sisi ndio tulioteremsha mawaidha
haya (Qur’an) na hakika Sisi ndio tutakayoyalinda” (15:9).
“Hakitakifikia batili mbele yake wala
nyuma yake, kimeteremshwa na Mwenye Hikima ahimidiwaye” (41:42).
§
Njia na
Hatua zilizotumika katika kuihifadhi na kuilinda Qur’an.
Mtume (s.a.w) mwenyewe aliweka misingi madhubuti ya kuihifadhi na
kuhakikisha kuwa Qur’an haipotei kupitia njia zifuatazo;
1.
Mtume (s.a.w) alihifadhishwa na kufanyishwa marejeo ya Qur’an
yote na Malaika Jibril (a.s) mara kwa mara, hasa mwezi wa Ramadhani.
Rejea Qur’an (73:1-4), (2:185).
2.
Mtume (s.a.w) aliahidiwa kuwa atasomeshwa Qur’an na
Mwenyezi Mungu (s.w) na hata sahau kamwe.
Rejea Qur’an (75:16-19) na (87:6-7).
3.
Mtume (s.a.w) aliwahifadhisha Maswahaba na Waislamu Qur’an
vifuani mwao wakati ilipokuwa inashuka.
Zaidi bin Thaabit amesema: “…..kila
nilipomaliza kuandika (Wahayi), Mtume (s.a.w) aliniamuru nisome nilichoandika
na nilikuwa ninamsomea. Kama palikuwa na kosa alilisahihisha kisha aliwapa
watu (kunakili na kuhifadhi vifuani mwao)”.
4.
Maswahaba waliihifadhi na kuisoma Qur’an mara kwa mara
hasa katika ibada za swala na zinginezo.
Rejea Qur’an (73:1-5).
5.
Mtume (s.a.w) aliwasomea waandishi wa Qur’an (wapatao
42) na kuandika kama walivyosomewa na kisha
Mtume (s.a.w) aliwataka wasome ili ahakiki walichoandika.
Uthman bin Affan (r.a) amesimulia:
“Wakati wowote Mtume wa Allah (s.a.w) alipoteremshiwa wahyi humuita mmoja wa
watu waliochaguliwa kuandika.” (Ameipokea Tirmidh)”.
6.
Mtume (s.a.w) aliwaagiza na kuwasimamia waandishi wa
Qur’an wapangilie sura na aya kama zilivyo
katika msahafu akiongozwa na Malaika Jibril (a.s).
Uthman bin Affan (r.a) ameeleza:
“Ilikuwa kawaida ya Mtume wa Allah kila iliposhuka aya za sura mbali mbali (za
Qur’an) au kila aya iliposhuka alimuita mmoja wapo wa waandishi wa Qur’an na
kumwambia, “andika aya hizi katika sura kadhaa baada ya aya kadhaa.”
§ Umihimu wa kunakiliwa upya Qur’an wakati wa
Uthman bin Affan (r.a).
Khalifa Uthman bin Affan (r.a) aliteuwa waandishi 4 kunakili misahafu 7
kutoka kwenye msahafu ulioandikwa wakati wa Mtume (s.a.w) kwa sababu zifuatazo;
- Kutokana na
kupanuka Dola ya Kiislamu na kusambaa maswahaba na walimu wa Qur’an maeneo
mbali mbali.
- Kuwa na
hitajio kubwa la kufundishwa ujumbe wa Qur’an sehemu mbali mbali hasa za
ugenini.
- Watu wengi waliingia katika Uislamu
wakiwa wageni wa lugha ya Qur’an (Kiarabu) na kushindwa kuisoma na kupata
ujumbe wa Qur’an.
- Kuepusha
kutofautiana kwa matamshi ya usomaji wa Qur’an ya asili katika ufikishaji wa
ujumbe wa Qur’an.
- Kuepusha
kupatikana mwanya wa maadui wa Uislamu katika upotoshaji na upoteaji wa ujumbe wa
asili wa Qur’an.