Jumatatu, 10 Aprili 2017

WAJIBU WA WAZAZI KWA MATOTO WAO KATIKA UISLAMU

         


                             WAJIBU WA WAZAZI KWA MATOTO WAO
Wazazi wanawajibu kwa watoto wao. Wajibu wa wazazi kwa watoto
wao ni kuwapa malezi bora yatakayowawezesha kuinukia kuwa watu wema
katika jamii watakao simamisha Ukhalifa katika ardhi. Malezi yanahusu yale
yote anayofanyiwa mtoto tangu akiwa tumboni mwa mama mpaka kufikia
umri wa kujitegemea. Wazazi wote wawili wanahusika kwa ukamilifu na
malezi haya. Malezi ya mtoto tunaweza kuyagawa katika sehemu mbili -
Malezi ya kimwili na malezi ya kimaadili.



                          Malezi ya kimwili:
Malezi ya kimwili ni yale yote anayofanyiwa mtoto ili akue katika afya
njema. Malezi haya huanza mara tu mama anapoanza ujauzito. Baba ana
wajibu wa kumtunza mkewe na kumpatia vyakula maalum ili mama na mtoto
wake tumboni wawe na afya nzuri. Jukumu la mama ni kufuata masharti ya
kulea mimba anayopewa na Daktari. Baada ya mtoto kuzaliwa wajibu wa
baba na mama kwa mtoto wao unabainishwa katika Qur-an:
Na wanawake waliozaa wawanyonyeshe watoto wao miaka
miwili kamili, kwa anayetaka kukamilisha kunyonyesha; na ni
juu ya baba chakula chao (mama na mtoto wake) na nguo zao
kwa sheria. Wala haikalifishwi nafsi yoyote ila kwa kadri ya
wasaa wake. Mama asitiwe taabuni kwa ajili ya mtoto wake,
wala baba (asitiwe taabuni) kwa ajili ya mtoto wake. Na juu ya
mrithi ni kama hivyo. Na wote wawili wakitaka kumwachisha
ziwa (kabla ya miaka miwili) kwa kuridhiana na kushauriana,
basi si kosa juu yao. Na kama mkitaka kuwapatia watoto wenu
mama wa kuwanyonyesha (wengine wasiokuwa mama zao) basi
haitakuwa dhambi juu yenu kama mkitoa (kuwapa hao
wanyonyeshaji) mlicho waahidi kwa sharia. Na mcheni
Mwenyezi Mungu na jueni kwamba Mwenyezi Mungu
anayaona yote mnayoyatenda. (2:233).
Aya hii inatubainishia wazi kuwa hata katika umri wa kunyonya
mtoto, wazazi wote wawili wanawajibika, kila mmoja katika nafasi yake.
Katika kipindi chote cha kumlea mtoto jukumu kubwa la baba ni kuilisha
familia, kuivisha na kuiweka katika makazi mazuri kwa kadiri ya wasaa
wake. Mama naye ana jukumu la kuwatunza watoto kwa kuhakikisha
kuwa wanakula vilivyo, wanakuwa wasafi wa mwili na nguo na wanaishi
katika mazingira masafi. Haya ndiyo malezi ya kimwili ambayo
humuwezesha mtoto kuwa na afya nzuri na kukua vyema.

                             Malezi ya Kimaadili:
Malezi ya kimwili ni muhimu sana, lakini yenyewe tu hayatoshelezi
kumuinua mtoto atakayekuwa raia mwema mwenye kuwajibika ipasavyo
kwa wazazi wake na jamii yake kwa ujumla.Uislamu haumtizami
mwanaadamu kama mnyama, bali unamtazama kama Khalifa wa Allah
(s.w) ambaye asili yake ni mwili unaotokana na udongo na roho takatifu
inayotokana na Allah (s.w) kama tunavyojifunza katika Qur-an:
Na (kumbuka) Mola wako alipowaambia Malaika: “Hakika
Mimi nitamuumba mtu kwa udongo mkavu unaotoa sauti,
wenye kutokana na matope meusi yaliyovunda! Basi
nitakapo mkamilisha na kumpulizia roho inayotokana na
Mimi, basi muangukieni kwa kumtii”. (15:28-29).
Kutokana na aya hizi tunajifunza kuwa kilichomfanya mwanaadamu
kuwa na hadhi juu ya viumbe vyote hata malaika ambao waliamrishwa na
Allah (s.w) kusujudiwa si uzuri wa sura yake au umbile lake, bali ni ile
Roho takatifu inayotokana na Allah (s.w). Lakini si kila mwanaadamu
atakayestahiki heshima hii ya kumsujudia na Malaika. Anayestahiki
heshima hii ni yule tu atakayeishi kwa kufuata tabia na mwenendo
anaoridhia Allah (s.w) au kwa kufuata maadili mema anayoyaridhia Allah
(s.w) na kufanya juhudi za kusimamisha Ukhalifa ardhi. Atakayeishi kwa
kufuata msukumo wa matashi ya mwili (unyama) wake na kuukataa
mwongozo wa Allah (s.w) na mtume wake atakuwa duni kuliko vilivyo
duni kama Allah (s.w) anavyotufahamisha:
Bila shaka tumemuumba mwanaadamu kwa umbo lililo bora
kabisa. Halafu tukamrudisha chini kuliko walio chini. Ila
wale wenye kuamini na kutenda mema, watakuwa na ujira
usio kwisha. (95:4-6).

Hivyo, wazazi sambamba na kuwalea watoto wao kimwili,
hawanabudi kuwalea kimaadili. Malezi hayo huanzia pale kwenye
kufanya tendo la ndoa (jimai) ambapo wazazi huleta dua ifuatayo:
Bismillah Allahumma jannib-na shaytwaani wajannibi shshaytwaani
maarazaqtanaa.
Kwa jina la Allah, Ee Allah muweke shetani mbali nasi na
muweke shetani mbali na hicho ulichoturuzuku".
Mimba inapotunga wazazi wa Kiislamu huomba dua, Allah (s.w))
awape mtoto mwema kama tunavyojifunza kaitka Qur'an ( 7:189)
Kila mtoto huzaliwa Muislamu, kama tunavyojifunza katika Hadith
ifuatayo:
Abu Hurairah (r.a) amesimulia kuwa Mtume wa Mwenyezi
Mungu amesema: "Hapana mtoto asiyezaliwa katika (dini
ya) asili (Uislamu). Kisha wazazi wake humfanya kuwa
Myahudi au Mkristo au Mmajusi. Amezaliwa kama
anavyozaliwa mnyama na miguu yake yote. Umemona
(mnyama) yeyote aliyezaliwa kilema? Kisha akasema:
"Umbile la Asili ndilo umbile Mwenyezi Mungu aliloumbia
watu. Hakuna mabadiliko katika maumbile ya viumbe vyote
vya Mwenyezi Mungu". (30:30) - (Bukhari na Muslim)
Hadith hii iliyomalizia na aya ya Qur'an (30:30) inatukumbusha kuwa
Uislamu ni dini ya maumbile inayolandana na umbile la binaadamu.
Kwahiyo, wazazi wa Kiislamu hawanabudi kumbakisha mtoto wao katika
dini yake ya asili kwa kufanya yafuatayo:
Kumuadhinia Mtoto
Mara tu mtoto anapozaliwa ni sunnah kumuadhinia sikio la kulia na
kumkimia kwa sikio la kushoto. Hekima yake ni kumuombea mtoto awe
mwema atakayesimamisha swala na kusimamisha Uislamu katika jamii.

                             Kumfanyia Mtoto Aqiqah
Ni sunnah vile vile kumfanyia mtoto aqiqah katika siku ya saba
baada ya kuzaliwa kwake. 'Aqiqah ni mbuzi anayechinjwa kwa ajili ya
mtoto aliyezaliwa anapofikia siku ya saba tokea kuzaliwa kwake. Sunnah
hii ya Aqiqah imetiliwa mkazo kwani Mtume (s.a.w) amesema:
Kila mtoto amefungika na aqiqah yake, itachinjwa kwa ajili
yake siku yake ya saba na atapewa jina, na atanyolewa
kichwa chake." (Ahmad, An-Nasai).
Katika kumtafuta mbuzi wa 'aqiqah ni vema kuzingatia masharti
yafuatayo:
Awe na umri usiopungua mwaka mmoja, awe bora kwa sura na
siha na asiwe na kilema chochote.
Ni sunnah vile vile kuigawa nyama ya aqiqah katika mafungu
yafuatayo:
- Theluthi ya kwanza watakula watu wa familia ya mtoto.
- Theluthi ya pili itatolewa sadaqa kwa mafakiri na maskini.
- Theluthi ya tatu itatolewa zawadi kwa majirani, marafiki na jamaa
wa karibu.
Ni sunnah kwa mtoto wa kiume afanyiwe Aqiqah kwa kuchinjiwa
mbuzi wawili. Pia ni sunnah siku hiyo ya saba anyolewe nywele na
zipimwe na kulinganishwa na uzito wa dhahabu au fedha, na kutolewa
sadaqa kulingana na uzito huo wa dhahabu au fedha.
Kama haikuwezekana kumfanyia mtoto aqiqah siku ya saba
unaweza kumfanyia siku ya kumi na nne (14) au siku ya ishirini na moja
(21).
Hekima ya kumfanyia mtoto aqiqah, ni kumshukuru Allah (s,w) kwa
kukuneemesha mtoto na kumuombea mtoto huyo kwa Allah kuwa
amuhifadhi na kumchunga na mabaya na amfanye mja mwema
atakayekuwa tayari kujitoa muhanga kwa mali na nafsi kwa ajili ya
kusimamisha Uislamu katika jamii.

                Kuwapenda na Kuwahurumia Watoto
Jambo jingine muhimu kwa wazazi katika kuwalea watoto wao ni
kuwa na upendo na huruma juu yao. Ukali wa kupindukia na ukaripiaji wa
mara kwa mara si malezi mazuri na kamwe mtoto haleleki vyema katika
mazingira kama hayo. Mtume (s.a.w) aliye kiigizo chetu, alikuwa ni mlezi
mwema mno. Alikuwa na huruma na upendo mkubwa mno juu ya watoto
wake na wajukuu zake kama tunavyojifunza katika Hadith zifuatazo:
Aysha (r.a) amesimulia: Sijamuona mtu aliyeshabihiana kitabia
na mwenendo na Mtume (s.a.w) kuliko Fatma. Alipokuja kwa
Mtume (s.a.w), Mtume (s.a.w) alimsimamia, kisha alimchukua
kwa mkono wake na kumbusu na kisha kumkalisha karibu yake.
Na Mtume (s.a.w) alipokwenda kwake, Fatma alikuwa
akimsimamia, kisha akimtwaa kwa mkono wake na kumbusu, na
kumkalisha karibu naye. (Abu Daud).
Pia Mtume (s.a.w) amesisitiza kuwapenda na kuwahurumia watoto
kwa kuwabusu kama Hadith zifuatazo zinavyotufahamisha:
Abu Hurairah ameeleza kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu
alimbusu mjukuu wake, Hassan bin Ali, mbele ya Aqra bin
Habis ambaye alisema: Nina watoto kumi na sijambusu hata
mmoja wao. Mtume wa Mwenyezi Mungu alimwangalia na
kusema: "Yule asiye na huruma hatahurumiwa". (Bukhari
na Muslim).
Aysha (r.a) ameeleza kuwa Mwarabu wa jangwani (Bedui)
alikuja kwa Mtume (s.a.w) akasema: Nini! Unabusu watoto?
Sisi hatuwabusu. Mtume (s.a.w) akasema: "Sina la
kuwasaidia, kwani Mwenyezi Mungu (s.w) ameondoa
huruma nyoyoni mwenu." (Bukhari na Muslim)
Hadith hizi mbili zinatusisitiza tuwalee watoto wetu kwa huruma na
upendo. Kuwabusu watoto ni kielelezo cha upendo wetu kwao.

                      Kuwaelimisha Watoto
Watoto wafunzwe tabia ya Kiislamu tangu mwanzo hasa pale
anapoanza kuongoea na kuelewa lile analoelekezwa. Watoto wafikiapo
umri wa miaka minne - mitano, wahudhurishwe pamoja na watoto
wenzao kwenye vituo vya malezi vya Kiislamu. Watoto wafunzwe namna
ya kuishi Kiislamu kwa kadiri ya umri wao. Wakifikia umri wa miaka saba
wazoeshwe kutekeleza ibada maalumu kama vile swala na swaumu.
Watoto wa miaka kumi na kuendelea walazimishwe kutekeleza
maamrisho yote ya Allah (s.w) kwa kadiri ya uwezo wao na kukatazwa
kuacha makatazo yake yote. Wakikaidi waonywe na kupewa adhabu

                    Kuwapa Watoto Nasaha
Watoto wetu wanapokuwa wakubwa tuwaozeshe mapema kwa
wanaume au wanawake wenye mwenendo na tabia ya Kiislamu na daima
tusiache kuwapa nasaha njema. Hebu turejee Qur-an tuone nasaha ya
Luqman kwa mwanawe:
Na (wakumbushe) Luqman alipomwambia mwanawe; na
hali ya kuwa anampa nasaha. Ewe mwanangu!
Usimshirikishe Mwenyezi Mungu, maana kushirikisha ndiyo
dhulma kubwa.(31:13)
Ewe mwanangu! Kwa hakika jambo lolote lijapokuwa na
uzito wa chembe ya hardali, likawa ndani ya jabali au
mbinguni, au katika ardhi, Mwenyezi Mungu atalileta bila
shaka Mwenyezi Mungu ni Latifu (Mpole), Mjuzi wa kila
jambo.(31:16)

Ewe Mwanangu! Simamisha swala, na uamrishe mema, na
ukataze mabaya, na usubiri juu ya yale yatakayokusibu.
Hakika hayo ni katika mambo yanayostahiki
kuaizimiwa.(31:17)
Wala usiwatazame (watu kwa jeuri) kwa upande mmoja wa
uso, wala usiende katika ardhi kwa maringo; hakika
Mw e n y e z i M u n g u h a m p e n d i k i l a a j i v u n a e ,
ajifaharishaye.(31:18)
Na ushike mwenendo wa katikati, na uteremshe sauti yako,
bila shaka sauti ya punda ni mbaya kuliko sauti zote (mbele
ya Mwenyezi Mungu (s.w).(31:19)
Pia turejee nasaha za Nabii Ibrahimu (a.s) na Ya'aquub (a.s) kwa
wana wao katika aya zifuatazo:
" (Kumb u k e n i h a b a r i h i i ) M o l a w a k e ( I b r a h imu )
alipomwambia: Aslim (Nyenyekea); akanena 'Nimenyenyekea
kwa Bwana mlezi wa walimwengu (wote) (2:131)
53
"Na Ibrahimu akawausia haya wanawe; na Ya'aquub!
Hakika Mwenyezi Mungu amekuchagulieni Dini hii (Al-
Islaam) basi msife ila mfe mkiwa Waislamu ". (2:132)

                               Tahadhari juu ya Watoto
Pamoja na kuwalea watoto wetu ipasavyo, hatuna budi kuchunga
mipaka ya Mwenyezi Mungu (s.w) katika kufanya kazi hiyo. Huruma na
upendo kwa watoto wetu kamwe kusitupelekee kwenda kinyume na
maamrisho ya Mwenyezi Mungu (s.w) na Mtume wake.Muislamu
anatakiwa ampende Mwenyezi Mungu (s.w) na Mtume wake kuliko hata
anavyoipenda nafsi yake, sembuse nafsi nyingine. Mara nyingi, baadhi
ya wazazi, kwa ajili ya kuwapenda na kuwahurumia watoto wao,
huwaachia huru kwenda kinyume na maamrisho na makatazo ya
Mwenyezi Mungu (s.w). Juu ya hili Allah (s.w) anatunasihi:
Enyi mlioamini! Yasikusahaulisheni mali yenu wala watoto
wenu kumkumbuka Mwenyezi Mungu! Na wafanyao hayo,
hao ndio wenye kuhasirika(63:9).
Enyi mlioamini! Kwa yakini baadhi ya wake zenu na watoto
wenu ni maadui zenu, basi jihadharini nao…............ (64:14).
Bila shaka mali zetu na watoto wenu ni mtihani. Na kwa
Mwenyezi Mungu kuna ujira mkubwa kabisa. (64:15).

Mali na watoto ni pambo la maisha ya dunia. Na vitendo
vizuri vibakiavyo ndivyo bora mbele ya Mola wako kwa
malipo na tumaini bora. (18:46).
Pamoja na kuwapenda na kuwahurumia wake zetu na watoto wetu
na pamoja na kuipenda mali na vyote vingine vinavyopendeka, hatuna
budi kuhakikisha kuwa upendo wetu juu ya Mwenyezi Mungu (s.w) na
Mtume wake nakupigania dini yake unakuwa juu ya kitu chochote kile
kama Mwenyezi Mungu (s.w) anavyotutanabahisha tena katika aya
zifuatazo:
Enyi mlioamini! Msiwafanye baba zenu na ndugu zenu
kuwa vipenzi (vyenu) ikiwa wanastahabu (wanapenda)
ukafiri kuliko Uislamu. Na katika nyinyi atakayewafanya
h a o k uwa n d i o v i p e n z i v y a k e , b a s i h a o n d i o
madhalimu.(9:23)
Sema:Kama baba zenu na wana wenu na ndugu zenu na
wake zenu na jamaa zenu na mali mlizochuma, na biashara
mnazoogopa kuharibikiwa, na majumba mnayoyapenda, ni
vipenzi zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume wake
na kupigania dini yake, basi ngojeni mpaka Mwenyezi
Mungu alete amri yake, na Mwenyezi Mungu hawaongozi
watu maasi. (9:24).
Jambo jingine muhimu la kuzingatia zaidi katika kuwalea watoto ni
kutokuwa na upendeleo wala ubaguzi kati ya watoto. Wazazi
wanawajibika sawa kwa watoto wao wote na kila mtoto ana haki sawa na
mwengine katika kupendwa na kuhurumiwa na wazazi wake.