Benki za Kiislamu
Benki za Kiislamu ambazo hutoa huduma kama benki
nyingine zinaendeshwa katika msingi wa biashara na sio
ule wa riba. Benki za Kiislamu badala ya kukopesha kwa
riba, hutumia rasilimali zake kwa zenyewe kujihusisha
katika uzalishaji kwa kufuata misingi inayokubalika katika
Uislamu. Miongoni mwa misingi inayokubalika kwa
Muislamu au Benki ya Kiislamu kuingiza fedha zake katika
miradi ya biashara au uzalishaji ni hii ifuatayo:
(i) Mudharabah
Mudharabah ni makubaliano kati ya watu wawili au
zaidi ambapo mmoja au zaidi kati ya hao anatoa mtaji na
mwingine hushiriki kwa ukamilifu katika kuendesha na
kuongoza mradi wa uchumi. Faida itakayopatikana katika
mradi huo itagawanywa kulingana na makubaliano yao.
Hasara itakayotokana na mradi huo itakuwa ni ya mwenye
kutoa mtaji. Wengine hawatoi chochote kusaidia hasara
kwa sababu wameshatoa mchango wao wa hasara hiyo
kwa jasho walilolitoa katika shughuli ambayo haikuzaa
matunda bali hasara.
Benki za Kiislamu zinaingiza fedha zake katika miradi ya
uchumi kwa njia hii ya Mudharabah ambapo benki hutoa
mtaji kwa ajili ya miradi mbali mbali ya uchumi kwa
mapatano ya kupata kiasi (asilimia) fulani cha faida
itakayopatikana na kuwa tayari kulipa hasara
itakayopatikana.
(ii) Musharikah
Musharikah ni ushiriki kati ya watu wawili ambapo,
tofauti na Mudharabah wote wawili wanachangia mtaji na
kushiriki katika uendeshaji wa shughuli ya kiuchumi,
lakini si lazima watoe hisa sawa sawa, kwa makubaliano
ya kugawana faida na hasara kulingana na kiasi cha hisa
alichotoa kila mmoja wao. Kwa mtindo huu wa
“Musharikah” Benki ya Kiislamu inaingia katika
kuchangia mtaji, kuendesha na kusimamia mradi wa
uchumi na watagawana (faida au hasara) kulingana na
kiasi cha mtaji kila mmoja alichotoa.
(iii) Ijara-Uara wa Iktina
Huu ni utaratibu mwingine unaokubalika kisheria
ambapo mtu au benki inatumia fedha zake katika kukodi
vitu kama vile magari, majumba, ardhi, na kadhalika,
ambavyo vikifanyiwa kazi huzalisha mali na kutoa faida.
Benki za Kiislamu hujipatia faida kubwa kutokana na
mtindo huu.
(iv) Murabah
Huu ni utaratibu unaotumiwa katika kununua bidhaa
kwa wingi kwa ajili ya kuwauzia wafanya biashara ambao
waliofikiana kuwa bidhaa hizo zinunuliwe kwa ajili yao.
Benki kutokana na uwezo wake inapanga na wafanya
biashara kuwa inunue bidhaa nyingi kutoka ndani na nje
ya nchi kwa jina lake kisha iwauzie wafanyabiashara hao
kwa bei itakayoipatia benki faida. Pia benki kwa mtindo
huu inaweza kununua mazao ya wakulima na kuyauza
kwa walaji kwa faida.
(v) Muqaradha
Mtindo huu wa Muqaradha humruhusu mtu au benki
kununua “share” au “bonds” katika kampuni ya uzalishaji
kwa mapatano ya kugawana faida au hasara kulingana
na kiasi cha “share”.
Kwa kufuata mitindo hii katika kuingiza fedha zake
katika miradi ya uchumi, Benki za Kiislamu hupata faida
kubwa hata zaidi ya kipato cha riba kinachopatikana katika
benki za riba. Benki za Kiislamu nazo hugawa faida
inayopatikana kwa wateja wake walioweka fedha zao
kwenye benki.
Uzuri wa benki
za Kiislamu
Pamoja na benki za Kiislamu kutoa huduma
zinazotolewa na kila benki kama tulivyoziorodhesha huko
nyuma, kuna faida za ziada zinazopatikana kutokana na
benki hizi kama ifuatavyo:
Kwanza benki za Kiislamu huiokoa
jamii na uchumi
wake na madhara yote yanayosababishwa na riba.
Pili, Benki za Kiislamu
huwaingiza katika uchumi
na kuwainua hata wale ambao hawana hata rasilimali
yoyote kwa mtindo wa Mudharabah. Hivyo ni kwamba,
benki zinazoendeshwa kwa mikopo ya riba, haziwezi
kukopesha fedha zake kwa mtu yeyote asiye na rasilimali
yenye thamani sawa au zaidi ya mkopo ili atakaposhindwa
kulipa ifilisiwe rasilimali hiyo. Kwa mtindo huu wa mikopo
ya riba, ni matajiri tu wanaopata mikopo ya benki na
masikini wasio na rasilimali yoyote huachwa hivyo hivyo
na umasikini wao bila ya msaada kutoka benki wa
kuwainua kiuchumi.
Tatu, benki za Kiislamu
huinua uchumi wa jamii,
kutokana na umakini na tahadhari kubwa zinazochukua
katika kuchagua na kuendesha miradi mbali mbali ya
uchumi. Kwa kuwa benki zenyewe zinajiingiza katika
uchumi, zinahakikisha kuwa miradi zitakazoichagua ni
ile yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha faida kubwa na
yenye uwezekano mdogo wa
kusababisha hasara.