Kusimamisha Swala.
Maana ya Kusimamisha Swala Kusimamisha swala ni tofauti na kuswali. Kuswali ni kufanya vitendo vya swala kama vile kusimama, kurukuu, kuitidali, kusujudu, n.k.
Kusimamisha swala ni kuitekeleza swala kwa kuchunga na kutekeleza kwa ukamilifu yafuatayo:
(i) Sharti zote za swala.
(ii) Nguzo zote za swala.
(iii) Kuwa na khushui (unyenyekevu) wakati wote wa kutekeleza sharti na nguzo za swala.
Mtu akiswali bila ya kuzingatia na kutekeleza kwa ukamilifu mambo haya matatu, ataonekana kuwa kaswali, lakini atakuwa hajasimamisha swala na atastahiki kuadhibiwa vikali na Mola wake kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo: Basi adhabu kali itawathibitikia wanaoswali, ambao wanapuuza swala zao (kwa kutozisimamisha), ambao hufanya ria (107:4-6).
Kupuuza swala ni pamoja na kutotekeleza ipasavyo sharti za swala, nguzo za swala, na kutokuwa na unyenyekevu wakati wa kutekeleza sharti na nguzo za swala. Hivyo, swala inayokubalika mbele ya Allah (s.w) ni ile iliyosimamishwa kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo: Hakika wamefuzu waumini ambao katika swala zao ni wanyenyekevu. (23:1-2) Na ambao swala zao wanazihifadhi. (23:9) Kuhifadhi swala ni kutekeleza kwa ukamilifu sharti na nguzo zote za swala.