Alhamisi, 27 Septemba 2018

Namna ya kuswali sehemu ya 13,14



13. Dua kabla ya salamu

Ni sunnah kuleta dua kabla ya salamu. Dua hizi ni nyingi ila miongoni mwanzo ni

 Dua  aliyotufundisha Mtume (s.a.w) kwa msisitizo mkubwa kama tunavyofahamishwa katika Hadithi ya Muslim, iliyosimuliwa na Ibn Abbas, ni hii ifuatayo: Allahumma Inni-audhubika min-’adhaabi-lqabri,Wa-auudhubika min fitnatil masiihi-ddajjaal, Wa-auudhubika min fitnatil-mahyaa wal-mamaati, “Ee Allah najikinga kwako kutokana na adhabu ya kabr, na najikinga kwako kutokana na fitina za masiihi Ddajjaal na najikinga kwako kutokana na matatizo ya maisha na mauti.


Sijidat-Sah-wi (Sijda ya kusahau)

Sijdat Sah-wi ni sijidah anayoileta mtu kabla ya kutoa salaam ili kufidia kitendo cha sunnah alicho kisahau kwa mfano kusahau kukaa tahiyaatu ya kwanza.Vile vile mtu akisahau au akikosea jambo lolote ambalo halibatilishi swala kwa mfano akaswali rakaa tano badala ya rakaa nne kwa swala ya Adhuhuri. Kabla hajamaliza swala alete sijidat Sahau. Hivi ndivyo tunavyojifunza kutokana na Hadithi zifuatazo: Abdullah bin Mas’ud (r.a) amesimulia: Mtume wa Allah alituswalisha Adhuhuri rakaa tano.Tukamuuliza kama pameamrishwa na Mwenyezi Mungu kurefushwa swala akajibu, La! Tukamuambia: “Umetuswalisha rakaa tano. Akasema (Mtume): Mimi ni binaadamu kama nyinyi, nakumbuka kama mnavyokumbuka na nasahau kama mnavyosahau. Kisha akasujudu sijdah mbili zikawa ni fidia kwa kusahau. (Bukhari na Muslim).



 Muhimu:

Kumbuka kuwa sijda hii Mtume (s.a.w) aliileta baada ya kutoa salaamu na baada ya kukumbushwa. Abdullah bin Buhaymah (r.a) amesimulia kuwa Mtume (s.a.w) aliswalisha swala ya adhuhuri, akasimama baada ya rakaa mbili, alipomaliza swala akasujudu mara mbili huku akisema: “Allah Akbar” katika kusujudu na katika kuinuka, wakati amekaa kabla ya kutoa salaam, na watu wakasujudu pamoja naye. Hii ilikuwa ni kufidia ile tahiyyatu ya mwanzo aliyoisahau”. (Muslim)


14. kutoa salamu.

Kutoa salamu ni nguzo katika nguzo za swala. Ukamilifu wa kutoa salamu ni kusema “as-salaamu alykum warahmatullahi wabarakaatuh” salamu zipo mbili yakwanza utatoa upande wa kulia na ya pili utatoa upande wakushoto. Sifa ya kugeuka kwa kutoa salamu ni kuwa utageuka mpaka mashavu yawze kuonekana kwa mtu aliye nyuma.