Jumanne, 4 Februari 2020

KISA CHA NABII NUHU

NUHU (A .S )
Mtume aliyemfuatia Nabii Idrisa(a.s)katika Mitume waliotajwa katika  Qur-an  ni  Nabii Nuhu(a.s).  Nuhu(a.s)  ni  miongoni  mwa Mitume  wa  mwanzo  mwanzo  kabisa.  Kutokana  na  mabaki  ya kihistoria tunajifunza kuwa Nabii Nuhu na kaumu yake waliishi katika nchi ya Iraq.
Mazingira ya Jamii Aliyoikuta Nabii Nuhu (a.s)
Nabii Nuhu(a.s) aliwakuta watu wa jamii yake wakimshirikisha A l l a h ( s . w ) k w a  n a m n a  m b a l i  m b a l i  n a w a l i k u w a
wakiabudia masanamu waliyoyachonga na kuyapa majina ya Wadda ,Suwa ’a ,Yaghuutha ,Ya ’uuka na Nasraa . Kama tulivyofahamishwa katika Qur-an kuwa viongozi wa jamii ya kishirikina ambao walikuwa ndio wapinzani wakubwa wa ujumbe wa Nabii Nuhu waliwanasihi wafuasi wao:


“Msiache miungu yenu, wala msiwache Wadda wala Suwa’a wala Yaghuutha na Ya’uka na Nasraa.” (71:23).
Mtume(s.a.w) anatufahamisha katika Hadith kuwa Wadda na
wale  waliotajwa  pamoja  naye  walikuwa  ni  watu  wacha-Mungu
katika  jamii  yao.  Walipofariki,watu  wakaanza  kuyazungukia

55


makaburi yao na shetani akakichochea kizazi kilichofuata kuunda sanamu za watu hao.   Kwa kufanya hivyo walidhani wangeliweza kuwaiga vitendo vyao vyema kwa kuwa na taswira za watu hao daima katika akili zao. Kizazi cha tatu kilishawishika kirahisi sana kuwa  watu  hao  walikuwa  ni  miungu  wanaostahiki  kuabudiwa badala au pamoja na Allah(s.w). Masanamu yote yanayoabudiwa yana historia ya namna hii.
Wito wa Nabii Nuhu(a.s) kwa Watu Wake
Nabii Nuhu (a .s ) kama walivyofanya Mitume wote ,
aliwafundisha watu wake Tawhiid kuwa wamuamini Allah (s.w) kwa
kuzingatia ishara mbali mbali zilizowazunguka, na kwamba
wamuabudu yeye peke yake na wasimshirikishe na   chochote.
Aliwaonya juu ya adhabu kali itakayowafika iwapo hawatakoma
kumshirikisha  Allah(s.w)  na  miungu  wengine.Juu  ya  wito  wa
Nuhu(a.s) kwa watu wake Qur-an inatufahamisha:
“Tulimpeleka Nuhu kwa watu wake, naye akasema:   “Enyi watu wangu!  Muabuduni Mwenyezi Mungu.  Nyinyi hamna Mungu ila yeye.   Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya siku (hiyo) iliyo kuu.”   (7:59).

Mbinu za Da’wah Alizotumia Nuhu(a.s)
Katika  kufikisha  ujumbe  huu  kwa  watu  wake  Nuhu(a.s), alijitahidi kutumia mbinu mbali mbali ili wapate kumuelewa vizuri na kufuata  ipasavyo  ujumbe  aliowaletea.  Miongoni  mwa  mbinu alizozitumia ni hizi zifuatazo:
Kwanza  alitoa  hoja  kwa  watu  wake  za  kuonesha  haja  na umuhimu  wa  kumuamini  Allah(s.w)  na  kumuabudu  ipasavyo. Aliwatanabahisha:
56
Mumekuwaje hamuweki hishima ya Mwenyezi Mungu. Na hali yeye amekuumbeni namna baada ya namna? Je hamuoni jinsi Mwenyezi   Mungu   alivyoziumba   mbingu   saba   tabakatabaka(moja juu ya moja). Na Akakaufanya mwezi ndani yake uwe nuru na Akalifanya jua kuwa taa? Na Mwenyezi Mungu amekuotesheni katika ardhi, mimea. Kisha atakurudisheni humo na atakutoeni tena.Na Mwenyezi Mungu amekufanyieni ardhi kuwa busati  (kitu kizuri mlichotandikiwa). Ili mtembee humo katika njia zilizo pana. (71:13-20)

Pili aliwabashiria  malipo  au  jaza  watakayopata  endapo watamwamini na kumtii Allah(s.w) ipasavyo. Kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:


Akasema  (Nuhu)  Enyi  watu  wangu!    Kwa  hakika  mimi  ni mwonyaji niliyedhahiri kwenu.   Ya kuwa mwabuduni Allah na mcheni na mnitii.(71:2-3)


Atakusameheni  madhambi  yenu  na  atakuakhirisheni  (bila  ya balaa) mpaka muda uliowekwa... ..(71:4)
57


Atakuleteeni mawingu yanyeshayo mvua nyingi.  Na atakupeni mali na
watoto, na atakupeni mabustani na atakufanyieni mito.”   (71:11-12)

Tatu aliwakhofisha watu wake na adhabu ya Allah(s.w) ya hapa duniani na huko akhera, endapo watakataa kumuamini Allah (s.w) na kumuabudu ipasavyo:

Na  sisi  tulimpeleka (tulimtuma)  Nuhu  kwa  watu  wake,
(akawaambia): “Mimi kwenu ni Muonyaji anayebainisha (kila
kitu).    Ya  kwamba  msimuabudu  yoyote isipokuwa  Mwenyezi
Mungu tu; hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya siku (kubwa hiyo) inayoumiza.” (11:25-26)
“Hakika  sisi  tulimtuma  Nuhu  kwa  watu  wake,  ya  kwamba
waonye watu wako kabla ya kuwajia adhabu iumizayo.”   (71:1)
Nne aliwalingania usiku na mchana:
“Akasema (Nuhu): Ee Mola wangu:  Kwa hakika nimewalingalia watu   wangu   usiku   na   mchana,   lakini   wito   wangu haukuwazidishia ila kukimbia”   (71:5-6)

58


Tano, aliwalingania kwa njia ya muhadhara kwa sauti:


Tena niliwaita kwa jahari. (71:8)

Sita, aliwalingania kwa siri kwa kumuendea mmoja mmoja:


“Kisha nikawatangazia kwa kelele, tena nikasema nao kwa siri’.   (71:9)

Saba,aliwaweka watu wake wazi kuwa hakuwa anawalingania kwenye Dini ya Allah(s.w) kwa kutaraji malipo yoyote kutoka kwao bali alifanya hivyo kwa manufaa yao wenyewe.“Na sikutakini juu yake ujira, ujira wangu hauko ila kwa Mola wa walimwengu wote.”   (26:109)

Nane,alisubiri na kudumu kuwalingania kwa mbinu
zilizoainishwa kwa muda wa miaka   elfu kasoro hamsini (950).“Na bila shaka tulimtuma Nuhu kwa watu wake na akakaa nao
miyaka elfu kasoro hamsini, (wasikubali kumfuata), basi tufani
liliwafika, (wakaghariki), na hali walikuwa   madhalimu (29:14)

Waliomuamini Nabii Nuhu(a.s)
Waliomuamini Nuhu(a.s) walikuwa watu wachache tena wale waliokuwa wanyonge na dhaifu katika jamii. Uchache na udhaifu wa waumini ilitumiwa na makafiri wa wakati wake kama hoja ya kumkataa Nuhu kuwa si Mtume wa Allah(sw).

59
“Wakasema:   Je, tukuamini wewe hali ya kuwa wanyonge ndio wanaokufuata?   (26:111)

Uchache wa waumini waliokuwa pamoja na Nabii Nuhu(a.s) unadhihiri vizuri pale walipo weza kuenea kwenye safina ndogo iliyosheheni mizigo yao na jozi za wanyama mbali mbali kama tunavyojifunza katika aya ifuatayo:
“Hata  ilipokuja  amri  yetu  na  ardhi  ikaanza  kufoka  maji tulimwambia (Nuhu) Pakia humo (jahazini) jozi moja katika kila (nyama, jike na dume) na wapakie watu wako wa nyumbani kwako isipokuwa wale ambao imewapitia hukumu (ya Mwenyezi Mungu).     Na (wachukue wote) walioamini.”   Na hawakuamini pamoja naye ila wachache tu.”   (11:40)

Wapinzani wa Ujumbe wa Nabii Nuhu(a.s) na Vitimbi Vyao
Waliokuwa mstari wa mbele katika kupinga ujumbe wa Nabii Nuhu(a.s), ni viongozi wakuu wa jamii yake.


Wakuu wa watu wake wakasema:   Sisi tunakuona umo katika
upotofu (upotevu)   ulio   dhahiri (kwa   kutukataza   haya
tuliyowakuta nayo wazee wetu)”   (7:60)

Katika  kukataa  ujumbe  wa  Nabii  Nuhu(a.s),  viongozi  wa makafiri walitoa hoja dhaifu zifuatazo:
60
“Na  hapa  wakasema  wakubwa  wa  wale  waliokufuru  katika kaumu yake.  Hatukuoni ila ni mtu tu sawa nasi; wala hatukuoni ila wamekufuata wale wanaoonekana dhahiri kuwa ni dhaifu (wanyonge) watu, (wamekufuata) kwa fikira ya mawazo tu (bila kupeleleza vizuri)  wala hatukuoneni kuwa mnayo ziada juu yetu; bali tunakuoneni kuwa ni waongo.   (11:27)

Wakasema  wale  wakuu  waliokufuru  katika  watu  wake:
“Hakuwa huyu (Nuhu) ila ni mtu kama nyinyi.  Anataka kujipatia
ubora  juu  yenu.    Na  kama  Mwenyezi  Mungu  angependa
(kukufundisheni),   kwa   yakini   angateremsha   Malaika.
Hatukusikia haya kwa wazee wetu wa mwanzo.”   (23:24)


Hakuwa huyu ila ni mtu mwenye wazimu.   Basi mngojeeni hata muda (wake atakufa).” (23:25)

Kwa mujibu wa aya hizi makafiri walikataa Utume wa Nabii Nuhu(a.s) kwa Sababu:
 Alikuwa mtu kama wao.   Walitarajia kutumiwa Malaika.
 Waliomuamini walikuwa watu dhaifu kiuchumi na hadhi.
 Kwa upande mmoja, hawakuona faida yoyote iliyopatikana


61


kwa waumini kutokana na kuamini kwao na kwa upande mwingine, hawakuona hasara yoyote waliyoipata kutokana na huko kukufuru kwao.
 Walimuita Nabii Nuhu mwenda wazimu:


Kabla yao watu wa Nuhu walikadhibisha nao.  Walimkadhibisha mja wetu  na wakasema ni mwendawazimu, na akawa anatolewa maneno makali”.   (54:9)
   Na walimtishia kumuua:


“Wakasema:  Kama hutaacha, Ewe Nuhu (nasaha zako hizi), bila shaka utakuwa miongoni mwa wanaorujumiwa  (wanaopigwa kwa mawe mpaka wafe)”.   (26:116)

Msimamo wa Nabii Nuhu(a.s) Dhidi ya Makafiri
Pamoja na upinzani mkali alioupata kutoka kwa viongozi wa
makafiri, Nabii Nuhu(a.s) aliendelea kwa hima kulingania Dini ya
Allah(s.w) na kuuweka wazi msimamo wake kama ifuatavyo:“Wasomee habari za Nuhu alipowaambia watu wake:  Enyi watu
wangu!   Ikiwa kukaa kwangu na nyinyi na kukumbusha kwangu
Aya za Mwenyezi Mungu kunakuchukizeni, basi mimi nategemea
kwa Mwenyezi Mungu.   Nanyi kusanyeni mambo yenu na hao
washirika wenu.   (Kusanyikeni mje kunidhuru, mimi sijali).  Tena

62


shauri lenu hilo lisifichikane kwenu (fanyeniu kwa dhahiri; mimi sijali tu).   Kisha mpitishe kwangu (hilo mnalotaka kupitisha). Wala  msinipe  nafasi  (hata  kidogo.  Mimi  sijali,  namtegemea Mwenyezi Mungu tu).”   (10:71)

Nabii Nuhu(a.s) aliendelea kuwausia watu wake na kudhihirisha msimamo wake.


“Na enyi watu wangu!   Mimi sikuombeni mali juu ya (jambo)
hili;  sina  ujira  wangu  ila  kwa  Mwenyezi  Mungu;  na  mimi
sitawafukuza walioamini (kama mnavyotaka kwangu niwafukuze
hao madhaifu ndipo msilimu nyinyi watukufu.   Sitafanya hivyo);
maana wao watakutana na Mola wao (awalipe kwa mema yao na
mabaya yao).   Lakini mimi nakuoneni nyinyi ni watu mnaofanya
ujinga. (Mnakataa  kuifuata  haki  kwa  kuwa  imefuatwa  na
madhaifu)!   (11:29).

Kwa ufupi tunajifunza kuwa:
• Nabii Nuhu(a.s) hakumchelea yeyote au chochote katika
kulingania Dini ya Allah(s.w), bali alimtegemea Allah(s.w).
• Alilingania Dini ya Allah kwa kutarajia malipo kutoka kwake tu.
• Aliwapokea na kuwakumbatia wote waliomuamini bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Ushindi wa Nabii Nuhu(a.s) na Wale Walioamini Pamoja Naye.
Nabii Nuhu(a.s)alilingania Uislamu katika mazingira magumu ya
upinzani mkubwa bila ya kukata tamaa kwa muda wa miaka 950.
Alipoona kuwa viongozi wa makafiri wanazidi kuweka mikakati ya


63


kuzuia watu kusilimu kila uchao na kuwashinikiza kurudi kwenye ukafiri hata wale walioamini kwa kuwafanyia vitimbi mbalimbali, Nabii Nuhu(a.s) alilazimika kuomba msaada wa Allah(s.w) dhidi ya makafiri kama tunavyojifunza katika aya zifuatazo:“Na  (wakumbushe) Nuhu alipotulingania zamani  (kutuomba) nasi tukamuitikia, na tukamuokoa yeye na watu wake katika shida (msiba) kubwa hiyo.(21:76)
Na tukamnusuru juu ya watu waliozikadhibisha aya zetu.  Hakika wao walikuwa watu wabaya.   Basi tukawatotesha (gharikisha) wote.”   (21:77)Kabla yao kama tulivyoona watu wa Nuhu walikadhibisha nao.
Walimkadhibisha mja Wetu na wakasema ni mwendawazimu; na
akawa anatolewa maneno makali.    Ndipo akamuomba Mola
wake (akasema): “Kwa  hakika  mimi  nimeshindwa,  basi
ninusuru.(54:9-10)Mara tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayomiminika (kwa nguvu kabisa).   Na tukazibubujisha maji chemchem zilizo katika ardhi; na maji (ya juu na chini) yakakutana kwa jambo lililokadiriwa (na Mungu).(54:11-12)

64


Na Tukamchukua (Nabii Nuhu) katika ile(jahazi) iliyotenge
nezwa  kwa  mbao  na  misumari.  Ikawa  inakwenda  mbele  ya macho, (hifadhi) Yetu. Hii ni tunzo (tuzo) kwa yule aliyekuwa amekataliwa (amekanushwa).   (54:13-14)

Kutokana na aya hizi tunajifunza kuwa Nabii Nuhu(a.s) pamoja
na waumini wachache aliokuwa nao walipata ushindi mkubwa juu
ya makafiri waliokuwa wengi na uwezo mkubwa kwa msaada wa
Allah(s.w).  Allah(s.w)  alitumia  jeshi  la “maji”  kuwaangamiza
makafiri na akawanusuru waumini kwa jahazi. Hii inatukumbusha kuwa:


“Na majeshi ya mbingu na ardhi ni ya Mwenyezi Mungu; na
Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mwenye hikima.”   (48:7)
Kuangamia kwa Mtoto na Mke wa Nuhu(a.s)
Tukirejea Qur’an (11:36-48) na (23:26 -29) tunapata maelezo juu ya mchakato wa kuangamizwa makafiri na kuokolewa waumini katika  kaumu  ya  Nabii  Nuhu(a.s).  Pamoja  na  Nabii  Nuhu(a.s) kuahidiwa kuwa watu wake wa nyumbani watakuwa miongoni mwa watakaookolewa na gharka, mtoto wake alikataa kuingia kwenye jahazi(safina) na akawa ni miongoni mwa wenye kuangamia kama tunavyo jifunza katika aya zifuatazo.65
Na akasema(Nuhu):”Pandeni humo, kwa jina la Mwenyezi Mungu kuwe kwenda kwake na kusimamma kwake. Hakika Mola wangu ni mwingi wa kusamehe na mwingi wa kurehemu.
Ikawa hiyo (jahazi) inakwenda nao katika mawimbi kama milima.
Na Nuhu akamwita mwanawe aliyekuwa mbali amekataa kuingia
jahazini: “Ewe mwanangu! Panda pamoja nasi wala usiwe pamoja
na makafiri”. Na akasema  (huyo mtoto)”  “Nitaukimbilia Mlima
utakaonilinda na maji” Akasema(Nuhu): “Hakuna leo wa kulindwa
na  amri  ya  Mwenyezi  Mungu  isipokuwa  yule  atakayemrehemu
(Mwenyezi Mungu).” Mara mawimbi yakaingia baina yao na akawa
miongoni mwa waliogharikishwa. (11:41-43)
Baada  ya  gharika  kuisha,  Nabii  Nuhu(a.s)  Ilibidi  amuelekee Mola wake kutaka kujua ni vipi mwanawe amekuwa miongoni mwa walioangamia.


66
Na  Nuhu  alimuomba  Mola  wake (alipomuona  mwanawe
anaangamia) akasema: Ewe Mola wangu! Mwanangu ni katika
watu wa nyumbani kwangu (mbona anaangamia)? Na hakika
ahadi Yako ni haki; nawe ni mwenye haki kuliko mahakimu
(wote).”Akasema (Mwenyezi  Mungu):  “Ewe  Nuhu!  Huyu  si
miongoni  mwa  watu  wako.  Yeye  ni (mwenye)  mwenendo
usiokuwa  mzuri.  Basi  usiniombe  ambayo  huyajui.  Mimi nakunasihi usiwe miongoni mwa wajinga.” (Nuhu) Akasema: Ee Mola  wangu!  Mimi  najikinga  kwako  nisije  kukuombatena nisiyoyajua; na kama hutanisamehe na kunirehemu nitakuwa miongoni mwa watakaopata khasara.”(11:45-47)

Pia tunahamishwa juu ya kuangamia mke wa Nuhu(a.s) katika aya ifuatayo:

Mwenyezi Mungu amepiga  (anapiga)mfano wa wale wabaya
waliokufuru, ni mkewe Nuhu na mkewe Luti. Walikuwa chini ya
waja wetu wema wawili hao miongoni mwa waja wetu (wema)’
lakini(wanawake  hao),  waliwafanyia  khiana (waume  zao
watukufu hao) na  (waume zao hao) hawakuweza kuwasaidia

67


chochote mbele ya Mwenyezi Mungu na ikasemwa: “Uingieni Moto pamoja na hao wanaouingia.” (66:10)

Kuangamia kwa mtoto na mke wa Nuhu(a.s) pamoja na mke wa Lut(a.s)  tunajifunza  kuwa  mtu  hataokoka  na  ghadhabu  ya Allah(s.w) kutokana a unasaba alioonao na watu wema na wala hata  faidika  na  malipo  ya  amali  njema  walizofanya  wengine. Kinyume chake hataadhibiwa mtu mwema kwa kuwa na unasaba na   watu   waovu   maadamu   anawafikishia   ujumbe   na wakamkanusha   kama   tunavyopigiwa   mfano   wa   mke   wa firaun,aliyekuwa mcha-mungu.


Na  Mwenyezi  Mngu  amepiga, (anapiga)  mfano  wa  wale
walioamini  kweli,  ni  mkewe  Firauni,  aliposema; “Ee  Mola
wangu! Nijengee nyumba Peponi karibu yako na uniokoe na
Firauni  na  amali  zake (mbovu),  na  Niokoe  na  watu
madhalimu”(66:11)
Mafunzo Yatokanayo na Historia ya Nabii Nuhu(a.s)
(i) Tuanze kulingania kwa Tawhiid - kumjua Allah(s.w)fika na
kumuabudu ipasavyo.
(ii)   Tulinganie kwa kutumia hoja na mbinu mbalimbali
kulingana na mazingira na wakati.
(iii) Tutumie hoja kuonesha udhaifu wa hoja za makafiri
dhidi ya Uislamu.
(iv)  Tusimchelee yeyote au chochote katika kulingania na
kusimamisha Dini ya Allah(s.w).


68


(v)   Tulinganie Uislamu kwa kutaraji malipo kutoka kwa
Allah(s.w)pekee.
(vi)   Waumini hawana budi kushikamana pamoja katika
kulingania na kusimamisha Uislamu katika jamii.
(vii)   Mlinganiaji awe na subira na kutowakatia tamaa wale
anaowalingania - Nabii Nuhu(a.s) alilingania miaka 950
na kupata wafuasi wachache sana bila ya kukata tamaa.
(viii) Mlinganiaji amuombe Allah(s.w) na kutegemea
msaada kutoka kwake.
(ix)   Hatanusurika mtu muovu na adhabu ya Allah(s.w)
kutokana na nasaba yake na Mitume wa Allah(s.w) na watu wema.
(x)   Hatima ya makafiri ni kuhiliki katika maisha ya dunia na
akhera.“Wala wale waliokufuru wasifikiri kwamba wao wamekwi
shatangulia (mbele, Allah hawapati), la, wao  hawatamshinda (Mwenyezi Mungu).   (8:59).
(xi)  Hatima ya waumini wanaharakati ni kuwashinda maadui
zao hapa ulimwenguni na kupata pepo huko akhera.
(xii)   Kushindwa na kuhiliki kwa makafiri wenye nguvu kubwa
za kijeshi na kiuchumi na waumini wachache na dhaifu
kijeshi nakiuchumi ni alama ya kuwepo Allah(s.w)
aliyoahidi kuwatawalisha katika ardhi waumini
wanaharakati.(Qur-an 24:55).
(xiii)  Siku zote wanaoongoza katika upinzani ni viongozi wa
kikafiri(matwaghuti).

69


(xiv)  Hatuna mtu atakaye epukana na ghadhabu za Allah(s.w)
na kupata pepo kwa amali njema alizofanya mtu
mwingine hata akiwa na unasaba au urafiki wa karibu
kiasi gani. Mtoto na mke wa Nuhu(a.s) waliangamia
kutokana na matendo yao maovu.
(xv)  Hakuna mtu atakaye adhibiwa kwa maovu ya mwingine
na huku akiwa ni muumini mtenda mema.   Mkewe Firaun
ni miongoni mwa wanawake wema waliotajwa katika
Qur’an.