Muhammad
Al-Ma’awy
Ulimwengu
wetu wa sasa umekuwa ni wa utandawazi (ulimwengushi) kwa kiasi ambacho yaliyo
ndiyo yamekuwa siyo na ya makosa yamechukuliwa kuwa ni ya makosa. Ulimwengu
umekuwa ukipigwa makombora na vyombo vya habari kwa njia moja au nyingine.
Mwenye
kumiliki chombo cha habari cha kilimwengu anaweza kupeperusha au kuandika ya
kwake na yakaweza kuchukuliwa kama ukweli mtupu. Ulimwengu umekuwa ni wenye
kuchukua yote na wenye sauti kubwa kwa kuwa na vyombo hivyo wameweza kusikika
mbali japokuwa hawana haki wa kupata wanayopata.
Kadhiya
moja ambayo imeeleweka sivyo ni kadhiya ya historia ya Palestina. Waliojizatiti
kuiweka katika hali hiyo iwe hivyo ni WAZEYUNI bila kuwa na
pingamizi kwa kuwa na sauti kubwa. Juhudi dhidi yao zimekuwa zikifanywa bila
ufanisi wowote kwa sababu ya sauti kubwa waliyonayo wao. Taasisi kubwa na
maarufu za vyombo vya habari zinamilikiwa nao kwa namna moja au nyingine. Mbali
na hiyo hatufai kufa moyo kuhusu juhudi hizo kwani nusura hutokea baada tawfiki
ya Allaah Aliyetukuka, kisha juhudi zetu kwa kutumia njia tofauti.
Kwa
sababu ya sifa zake Palestina, kama hali ya hewa, rutuba ya ardhi na
upatikanaji wa maji safi ndio wavamizi wengi wamejaribu kuiteka ardhi hii na
kuitawala kimabavu.
Makao
ya awali yalianzishwa Palestina katika miaka ya 14000 hadi 8000 KI (Kabla ya
kuzaliwa kwa ‘Nabii ‘Iysa) kwa utawala wa Tatwafi. Na katika mwaka 8000 KI, mji
wa Ariha (Jericho) ulianzishwa huko Palestina. Mji huo ulijengwa na wenyeji
ukajengeka kwa njia ya mipango kama ilivyo miji ya kisasa.
Makabila
ya mwanzo kuja kuweka makazi yao katika nchi ya Palestina ni yale makabila ya
Wayebusi, Waamori, Wahiti, Wakanaani, Waamalika na Wafiniki. Makabila haya
yalikaa katika maeneo tofauti ya nchi hiyo: Wakanaani waliweka makazi yao
katika eneo la Gaza ilhali Wayebusi walibuni mji wa Yebus, ambao kwa sasa
unajulikana kama mji wa al-Quds. Makabila haya yalihamia huko kutoka kusini mwa
Bara Arabu takriban mwaka 3000 KI.
Katika
mwaka wa 1900 KI, Nabii Ibraahim (‘Alayhis Salaam) alihamia kutoka Iraq na kuja
kuweka makazi yake katika mji wa Khalil. Hapo ndipo alipomzaa Nabii Ismaa‘iyl
na Ishaaq (‘Alayhimas Salaam) na baadaye kuzaliwa Nabii Ya‘quub (‘Alayhis
Salaam).
Katika
kipindi 1800 – 1600 KI, Palestina ilitawaliwa na Waheksosi. Ni katika kipindi
hiki katika mwaka wa 1750 KI ndio Nabii Ya‘quub (‘Alayhis Salaam) alizaliwa.
Katika
karne ya 16 KI (yaani mwaka wa 1580 KI), Bani Israili waliokuwa Misri walitiwa
utumwani na Firauni wa wakati huo kuvamia na kuitawala Palestina kwa muda kabla
ya sehemu hiyo kuingia katika utawala wa Kiislamu.
Mwaka
1250 KI, Nabii Musa (‘Alayhis Salaam) aliagiziwa na Allaah Aliyetukuka atoke
Misri ambako wana wa Israili walikuwa ni watumwa waende wakaishi katika ardhi
tukufu. Kwa ajili ya ukaidi wao (Qur-aan 5: 21 – 26), walipigwa marufuku
kuingia katika ardhi hiyo. Mbali na hilo walipigwa adhabu kali ya kutangatanga
katika jangwa kwa muda wa miaka arobaini (40). Katika kipindi hicho, wale wote
waliokuwa wamebaleghe walikufa katika jangwa kikabakia kizazi ambacho
kililelekea katika maadili ya Kiislamu, Imani na uchaji Allaah kuingia
katika ardhi hiyo tukufu. Kizazi hicho kilipata darsa ya ukakamavu, utii,
kujitolea mhanga na malezi bora, hivyo kwa tawfiki ya Allaah Aliyetukuka kuweza
kuingia ardhi hiyo mwaka 1190 KI wakiongozwa na Yusha bin Nuun (‘Alayhis
Salaam). Wakati huo tayari Nabii Muusa (‘Alayhis Salaam) alikuwa ameaga dunia
hivyo kutoweza kuingia katika ardhi hiyo.
Yusha
bin Nuun (‘Alayhis Salaam) ndiye mwana Israili wa kwanza aliyeanzisha dola
katika maeneo ya Palestina. Hata hivyo, wana wa Israili chini ya uongozi wa
Yusha bin Nuun (‘Alayhis Salaam) hawakuweza kuliteka eneo lote la Palestina
katika mipaka yake ya sasa na hata mji wa al-Quds haukuingia mikononi mwake.
Ifahamike kuwa dola hiyo haikuwa katika misingi ya Kiyahudi kwani dini ya
Kiyahudi ilikuwa haijabuniwa kamwe wakati huo bali ilikuwa ikipekeshwa katika
misingi ya Kiislamu.
Dola
hii haikukaa kwa muda kwani vurugu liliingia kati baada ya kuaga dunia Yusha
bin Nuun (‘Alayhis Salaam), hivyo kushikiliwa na Ma-Qaadhi kabla ya
kusambaratika kabisa kabisa. Kufikiwa na hayo, Bani Israili waliingia katika
utawala wa Wapalestina ambayo asili yao ni Wakanaani. Kudhalilishwa kwao huko
kuliwafanya watake msaada kutoka kwa Allaah Aliyetukuka ili warudi katika enzi
zao (Qur-aan, 2: 246). Allaah Aliyetukuka Aliwateulia Twaaluut kuwa mfalme wao
wa kuwaongoza wao kwenda kupambana na Wapalestina wakiongozwa na Jaaluut
(Qur-aan, 2: 247). Bani Israili waligomba sana kuhusu uchaguzi huo, hata hivyo
wapo waliokuwa na Imani ambao walisalimu amri na kujizatiti kwenda
kupambana na Wapalestina. Wakati huo, Nabii Daawuud (‘Alayhis Salaam) alikuwa
kijana mdogo aliyejiunga na jeshi hilo ambalo kwa tawfiki ya Allaah Aliyetukuka
liliweza kulishinda jeshi la Jaaluut (Qur-aan, 2: 248 – 251). Ushindi huo
ulipatikana mwaka wa 1025 KI. Twaaluut aliweza kuanzisha tena dola ya Kiislamu
Palestina ikiwa inaongozwa na Bani Israili mpaka kufa kwake mnamo 1004 KI.
Baada
ya kuaga dunia tu, hatamu za uongozi zilishikwa na Nabii Daawuud (‘Alayhis
Salaam) ambaye aliipanua dola hiyo kwa kasi kubwa sana. Ni wakati wake ndio mji
wa al-Quds uliweza kutekwa. Nabii Daawuud (‘Alayhis Salaam) aliaga dunia mwaka
wa 960 KI na kumuacha mtoto wake, Nabii Sulaymaan (‘Alayhis Salaam) katika
utawala. Kwa upande wake naye, Nabii Sulaymaan (‘Alayhis Salaam) aliipanua dola
hiyo lakini haikufika katika mipaka yake ya sasa. Nabii Sulaymaan (‘Alayhis
Salaam) aliimarisha sana dola hiyo, akiwa yeye na babake wameitawala kwa
misingi ya Kiislamu. Ilibaki hivyo hadi mwaka wa 922 KI pale naye alipoaga
dunia.
Kufariki
kwake kuliifanya dola hiyo igawanywe sehemu mbili: Dola ya Yuda (kusini)
na Kizeyuni (kaskazini). Bani Israili waligawanyika katika koo zao kwa
kiasi ambacho walianza kupigana wao kwa wao (baina dola mbili hizo) na ufisadi
ukakithiri kwa kiasi kikubwa sana. Wakati huo ndio alitokea mtu kwa jina la
Yuda aliyekiuka mipaka ya Dini na kuasi. Alipata wafuasi wengi na hapo
kukazaliwa Dini ya Uyahudi.
Hali
hiyo halisi ya mapambano baina ya Bani Israili iliwapelekea dola zao mbili hizo
kudhoofika na mwisho katika mwaka wa 722 KI, dola ya Israili ilianguka na eneo
hilo kutawaliwa na Wa-Asiria. Nayo dola ya Yuda ilivamiwa na mfalme Nubukadneza
wa Babeli (Iraq) mwaka 586 KI, na dola hiyo kuingia katika utawala wa Kibabeli.
Wana wa Israili wote walipelekwa uhamishoni huko Iraq kama watumwa. Hapo
wengine wao walipata kukimbia na kuingia Ufursi (Iran) ambapo walijaribu
kufanya mahusiano ya karibu na utawala wa huko hadi wakamtoa msichana wao kwa
ajili ya kuolewa na mfalme wa Iran. Mafungamano hayo yalimfanya mfalme Cyrus wa
Iran aunde jeshi kwa usaidizi wa Mayahudi ili kuivamia Palestina na kuwang’oa
Wababeli. Cyrus alifanikiwa kuwashinda Wababeli kutoka Palestina na kuwapatia
ruhusa Mayahudi kurudi katika nchi hiyo lakini hata hivyo waliorudi hawakuwa
wengi, walikuwa wachache sana. Wengi miongoni mwao walibakia katika nchi ya
uhamisho wao. Kushinda kwao kulitokea mwaka wa 538 KI. Hata hivyo, Mayahudi
wakati wa utawala wa Kifursi hawakuwa na mamlaka wala madaraka yoyote lakini
walipatiwa uhuru wa kufanya Ibadah zao bila kufuatiliwa, kuingiliwa wala
kubughudhiwa na Wafursi.
Na
katika mwaka 332 KI, Palestina ilivamiwa na kutekwa na Warumi wakiongozwa na
Alexander kutoka Macedonia. Hata hivyo, Warumi hawakuweza kukaa huko kwa muda
mrefu pale wafalme wa kutoka Syria walipovamia sehemu hiyo na kuitia katika
utawala wao mwaka 198 KI.
Wayunani
nao waliiteka ardhi hiyo mwaka wa 175 Ki na kuitawala. Mayahudi waliweza
kujizatiti na kuiteka sehemu hiyo ya ardhi mwaka wa 166 KI na ikabaki mikononi
mwao kwa kipindi cha miaka 4. Wasyria walirudi tena kwa kishindo na kuwashinda
Mayahudi mwaka wa 162 KI. Hata hivyo, nao Mayahudi walijizatiti kwa mara nyingine
tena wakaja wakawang’oa Wasyria kutoka sehemu hiyo mwaka 143 KI. Hapo waliweza
kuibakisha ardhi hiyo katika utawala wao hadi mwaka 70 KI.
Kwa
miaka saba baada ya huo mwaka wa 70 kukawepo vurugu kubwa hadi mwishowe Warumi
wakaweza kuwashinda Mayahudi mnamo 63 KI. Kuanzia mwaka huo hadi mwaka wa 616
BI (Baada ya kuzaliwa kwa Nabii ‘Iysa) Palestina ilibaki katika utawala wa
Warumi isipokuwa kile kipindi cha mapinduzi ya Mayahudi cha mwaka 66 BI na 132
– 135 BI. Hata hivyo, katika kipindi cha mapinduzi hayo ya Mayahudi serikali ya
Roma ilituma wanajeshi wake wengi ili kuyasagasaga hayo mapinduzi. Ni wakati
huo ndio serikali ya Kirumi ilipitisha sheria kuwa mji wa al-Quds haufai
kukaliwa na Mayahudi.
Utawala
wa Kirumi ulisitishwa kidogo na ule wa Wafursi mwaka wa 616 BI. Lakini utawala
wa Wafursi haukukaa kwa muda mrefu kwani katika mwaka wa 624 BI walishindwa na
Warumi katika vita ambavyo Allaah Amevizungumzia katika Suratur Ruum (30):
Aayah 1 – 5. Warumi waliweza kusonga mbele hadi kuuteka mji wa al-Quds katika
kipindi cha muda miaka 3 hadi 4.
Kipindi
baada ya Sulhu ya Hudaybiyah ndicho kile ambacho Mtume Muhammad (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) alianza kupeleka barua kwa mataifa mbali
na ndio barua hiyo ikamfikia mfalme wa Warumi, Hiraql (Heraclius) akiwa al-Quds
mwaka wa 628 BI. Hapo ndio yalianza mapambano baina ya Waislamu wakiongozwa na
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Warumi. Mji wa
al-Quds uliingia mikononi mwa Waislamu wakati wa ukhalifa wa 'Umar bin al-Khatwtwaab
(Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye alifunga safari kwenda kuchukua funguo za mji
kutoka kwa kasisi Sophronius mwaka wa 638 BI na hapo miji mingi ya Palestina
ikaingia katika Dola ya Kiislamu. Nchi hiyo pamoja na nchi za Shaam zote
zilibakia katika utawala wa Kiislamu hadi mwaka wa 1099 BI wakati ambapo
Wakristo walikuja kuzivamia ardhi hizo katika vita vya Msalaba.
Watu
wa Msalaba kutoka bara Ulaya waliweza kuwaua Waislamu 70,000 ndani ya eneo la
Msikiti wa Aqswa. Wakristo waliweza kuitawala ardhi hiyo kwa muda wa miaka 88
ambapo harakati za kuikomboa zilipamba moto. Harakati hizo zilianzishwa na
Nuurud-Diyn Zinkiy, mwanae Nuurud-Diyn Mahmuud na baadaye Swalaahud-Diyn Hasan
al-Ayyuubiy ambaye aliweza kwa tawfiki ya Allaah kuirudisha Palestina kuwa
katika Dola ya Kiislamu mwaka 1187 BI.
Kuanzia
mwaka huo wa 1187 BI, Palestina ilibakia kuwa katika Dola ya Kiislamu hadi
baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia (1917) ndio Palestina iliingia katika
utawala wa Uingereza. Wenyeji wa al-Quds hawakusadiki masikio yao pale
walipokusanyika kumsikiliza jemadari Allenby katika uwanja wa al-Quds. Allenby
alisema kwa uwazi kabisa: “Leo ndio vita vya Msalaba vimekwisha”. Kabla hata ya
kuiteka na kuitawala ardhi hiyo, serikali ya Uingereza tayari ilikuwa
imewaahidi Wazeyuni kuwa wakiondoka watawazawadia wao kipande hicho cha ardhi.
Hayo yanapatikana katika ahadi au tangazo la Waziri wa Nje, Arthur James
Balfour ya tarehe 2 Novemba 1917.
Na
kweli kwa ahadi yao, Uingereza ilipoondoka Mei 1948 waliwaachia ardhi hiyo
Wazeyuni wasiokuwa na mafungamano na ardhi hiyo. Hakika ni kuwa Mayahudi wakati
huo na kabla ya hapo hawakuwa na kitambulisho cha aina yoyote ile. Hii ni kwa
mujibu wa barua aliyoiandika Dkt Chaim Weizman ya 18 Aprili 1918 kwa mkewe: “Ni
masikitiko makubwa kuona kuwa hapa hatuna chochote. Hapa hakuna hata taasisi
moja ya Kiyahudi, lakini kumejaa minara (kumaanisha wingi wa Misikiti)”.
Ndugu
zetu walianzisha harakati ya kutaka kujikomboa na minyororo ya ukoloni.
Harakati ya kwanza ni ile iliyoongozwa na Sh. Abdul-Qaadir al-Qassaam, kutoka
Syria mwaka 1925. Mwaka wa 1929 kulikuwa na Intifadha ya al-Buraaq, naye Sh.
Al-Qassaam akauliwa mwaka wa 1935 alipokuwa anapambana na jeshi la Muingereza
katika maeneo hayo matakatifu.
Kuanzia
mwaka wa 1948, kumekuwa na vita baina ya Waarabu na Wazeyuni, lakini Waarabu
wakashindwa sana kwa kutokuwa na kuwa wamoja na kauli moja, kutokuwa na mipango
mizuri na wakati mwengine kushirikiana na dola haramu ya Kizeyuni. Hata hivyo,
sababu kubwa ya kushindwa ni kule Waarabu kuichukulia kuwa hiyo ni kadhiya ya
Waarabu tu na kutowajumuisha Waislamu wengineo.
MAREJEO
bofya hapa