Sala
ya Ijumaa
Imeitwa
Sala ya Ijumaa kwa vile inasaliwa siku ya Ijumaa, au kwa yale ya kheri yaliomo
kwenye siku hii. Sala ya Ijumaa ni bora yao ya Sala na siku ya Ijumaa ni bora
yao ya siku. Hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:
"Bora
ya siku zilizochomoza jua juu yake ni siku ya Ijumaa, siku hio ameumbwa Adam
a.s., na siku hio ametiwa Peponi, na siku hio ametoka Peponi, wala hakitasimama
Qiyama isipokuwa siku ya Ijumaa". (Imehadithiwa na Muslim na Abu Daud na
Al Nissaai na Al Tirmidhy).
Sala
ya Ijumaa ni waajibu kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, qauli ya Mtume s.a.w.
na itifaqi ya wanazuoni. Ametwambia Mwenyezi Mungu Mtukufu:
"Enyi
mlio amini! Ikiadhiniwa Sala siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye dhikri ya
Mwenyezi Mungu, na wacheni biashara ……". (Al Jumu'a : 9).
Na
amesema Mtume s.a.w.:
"Niliazimia
nimuamrishe mtu asalishe, kisha nende nikawachomee moto nyumba zao watu
wasiokwenda kusali Sala ya Ijumaa ". (Imehadithiwa na Muslim).
Na
katika upokezi mwengine:
"Wasiwache
watu kutekeleza Sala ya Ijumaa, wakiwacha Mwenyezi Mungu atapiga mihuri kwenye
nyoyo zao na hapo watakuwa miongoni mwa walioghafilika". (Imehadithiwa na
Muslim na wengineo).
Na
Hadithi nyengine ya Matume s.a.w.: "Kuiendea
Sala ya Ijumaa ni waajibu kwa kila balegh". (Imehadithiwa na Al Nissaai).
Na
Hadithi nyengine ya Mtume s.a.w.:
"Mwenye
kuwacha kusali Sala ya Ijumaa, Ijumaa tatu (mfululizo); Mwenyezi Mungu hupiga
muhuri kwenye moyo wake". (Imehadithiwa na Abu Daud na Al Tirmidhy na Al
Nissaai).
Shuruti
za kuwajibikia Sala ya Ijumaa ni saba:
Ya
Kwanza, Uislam, kama ilivyotajwa kwenye Kitabu cha Sala.
Ya
Pili mpaka ya Sita, kuwa huru, baalegh, mwenye akili kamilifu,
mwanamume, mzima wa siha. Hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:
"Sala
ya Ijumaa ni waajibu kwa kila Muislam, isipokua kwa watu wanne, mwenye
kumilikiwa, mwanamke, mtoto mdogo na mgonjwa". (Imehadithiwa na Abu Daud).
Mgonjwa
wa akili yeye si mwenye kukalifishwa na Sharia kwa lolote lile. Kwenye hukmu ya
ugonjwa imekisiwa kuingia, kukosa cha kusitiri utupu, kukhofu dhulma na
madhaalim, na mwenye tumbo la kuendesha na hawezi kujizuia; lau itakhofiwa
maiti kuharibika, watu wataacha kwenda
kusali
Sala ya Ijumaa na kumshughulikia maiti mpaka kumzika.
Ya
Saba, mkaazi, si msafiri; haimuwajibikii Sala ya Ijumaa msafiri. Hivi
ni kwa vile haikupokewa kuwa Mtume s.a.w. amewahi kusali Sala ya Ijumaa nae
yumo safarini, bali imepokewa kuwa: "Haimlazimu
Sala ya Ijumaa aliomo safarini". (Imehadithiwa na Al Bayhaqy).
Mbali
na shuruti za Sala tulizotangulia kuzitaja, kusihi Sala ya Ijumaa ina shuruti
tatu ziada:
Ya
Kwanza, iwe kwenye pahala wanapoishi idadi ya watu wenye kutimiza Sala
ya jama'a, kwa aina yoyote ile ya majengo.
Ya
Pili, isaliwe jama'a; haikuwahi kupokewa kwamba Mtume wetu Mpezni
s.a.w. au Makhalifa wa baada yake wamewahi kusali Sala ya Ijumaa mtu peke yake.
Idadi ya watu wenye kufanya jama'a ya kulazim Sala ya Ijumaa wasipungue watu
arubaini. Kwa Hadithi ya Jaabir r.a. kwamba:
"Imekuwa
ni mwenendo kwamba kila penye watu arubaini na zaidi (husaliwa) Sala ya
Ijumaa". Imehadithiwa na Al Bayhaqy).
Na
kwa Hadithi ya Ka'ab bin Malik r.a.:
"Mtu
wa mwanzo kutusalisha Sala ya Ijumaa kwenye kijiji cha Khudhamaat ni As'ad bin
Zaraara na tulikuwa watu arubaini". (Ibnu Hibbaan na Al Bayhaqy waimeipa
darja ya Hadithi sahih).
Na
kwa Hadithi nyengine kwamba Mtume s.a.w.:
"Mtume
s.a.w. amesali Sala ya Ijumaa akiweko Madina, wala haikupokewa kutoka kwake
kwamba alisali Sala ya Ijumaa kwa uchache ya watu arubaini".
Ya
Tatu, isaliwe kwenye wakati wake, wakati wake ni ule wakati wa Sala ya
adhuhuri. Hivi ni kwa qauli ya Anas r.a.:
"Mtume
s.a.w. alikuwa akisali Sala ya Ijumaa baada ya kutenguka jua".
(Imehadithiwa na Al Bukhary).
Imepokewa
kutoka kwa Salama bin Al Aku'i r.a.:
"Tulikuwa
tukisali Sala ya Ijumaa pamoja na Mtume s.a.w. linapotenguka jua".
Ikiwa
itakuwa dhiki ya wakati, ikawa haiwezekani kusaliwa Sala ya Ijumaa, basi
itasaliwa Sala ya adhuhuri badala ya Sala ya Ijumaa. Ikiwa wataingiwa na shaka
kama wakati umetoka au laa, basi watasali Sala ya adhuhuri, kwani kuhakikisha
kuweko wakati ni sharti ya kusihi Sala.
Fardhi
za Sala ya Ijumaa ni tatu:
Ya
Kwanza, itanguliwe na khutba mbili, baina ya khutba na khutba kitako.
Imepokewa kutoka kwa Jaabir bin Samra r.a. kwamba Mtume s.a.w.:
"Mtume
s.a.w. alikuwa akikhutubu khutba mbili na akikaa baina ya khutba mbili hizo, na
akikhutubu hali amesimama".
Imepokewa
vile vile:
"Hakika
ya Mtume s.a.w. alikuwa akikhutubu khutba mbili, akisoma Qur'ani na akiwaadhi
watu".
Nguzo
za Khutba ya Ijumaa
Khutba
ya Sala ya Ijumaa ina nguzo tano:
Kwanza, kumshukuru
Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Pili, kumsalia
na kumuombea Rehma Mtume s.a.w.
Tatu, kuusia
watu kumcha Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Nne, kuwaombea
du'a Waumini kwenye khutba ya pili.
Tano, kusoma
Qur'ani; uchache wake ni Aya kaamili.
Khutba
ya Sala ya Ijumaa ina shuruti saba:
Kwanza, kuingia
wakati wa Sala.
Pili, kutangulia
khutba mbili kabla ya Sala.
Tatu, kusimama;
kwa mwenye kuweza.
Nne, kukaa
kitako baina ya khutba mbili kwa kiasi cha kutulia.
Tano, ku'tahirika
na hadathi kubwa na ndogo na najsi (uchafu), mwilini, nguoni, na mahala
pakusalia.
Sita, kusitiri
utupu kwa nguo ilio 'taahir.
Saba, kutoa
sauti ya kusikilika na watu arubaini ambao wanalazimika na hii Sala.
Fardhi
ya Pili, isaliwe raka'a mbili; hivi ni kwa qauli ya Sayyidna 'Umar
r.a.:
Maana
yake ni kama hivi: "Sala ya Ijumaa ni raka'a mbili bila ya kupunguza, kama
alivyosema Mtume s.a.w.".
Fardhi
ya Tatu, isaliwe jama'a; tumeshataja dalili ya hivi.
Haiati
(Mapambo) ya Sala ya Ijumaa
Inasuniwa
kwa mwenye kwenda kusali Sala ya Ijumaa, mambo manne:
La
Kwanza, akoge, hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:
"Mwenye
kwenda kusali Sala ya Ijumaa basi naakoge". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).
La
Pili, asafishe kiwiliwili chake uchafu wenye kusababisha harufu mbovu
ya mwili, na hivyo ndivyo inavyokusudiwa kwa kusemwa akoge, sio basi ajimwagie
maji. Amesema Imam Shafi'ii r.a.:
"Mwenye
kunadhifisha nguo zake hupungua wasiwasi wake, na mwenye kufanya harufu yake
kuwa nzuri (kujitia manukato) huzidi akili yake".
La
Tatu, kujipamba kwa kuvaa nguo nzuri na kwa kujitia manukato. Hivi ni
kwa qauli yake Mtume s.a.w.:
"Mwenye
kukoga siku ya Ijumaa na akavaa nzuri mno ya nguo zake na akajitia manukato
kutoka nyumbani kwake - ikiwa anayo - kisha akenda kusali Ijumaa, akiingia
msikitini asikiuke watu waliokwishakaa (kutaka kwenda mbele), kisha akasali
alicho andikiwa, kisha akamsikiliza imam, mpaka akamaliza Sala yake; huwa ni
kafara kwake kwa kiliopo baina ya Ijumaa hii na Ijumaa
iliopita". (Imepokewa na Ibnu Hibban na Al Haakim).
Kuvaa
nguo nyeupe kwa kuhudhuria Sala ya Ijumaa ni bora zaidi. Hivi kwa qauli ya
Mtume s.a.w.:
"Vaeni
nguo nyeupe, kwani hizo ni bora mno ya nguo zenu; na kwa nguo nyeupe wakafinini
maiti wenu".
La
Nne, kukata kucha na nywele zenye kupendeza kuondolewa; kwani hivi ni
katika unadhifu.
Wamekhitalifiana
rai wanazuoni juu ya hukmu ya kuzungumza wakati wa khutba ya Sala ya Ijumaa.
Amesema Imam Shafi'ii r.a. na Imam Malik na Imam Abu Hanifa r.a. na Imam Ahmad
r.a. kwamba inaharimishwa kuzungumza wakati wa khutba ya Sala ya Ijumaa. Wao
wametolea hoja Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
"Na
isomwapo Qur'ani isikilizeni na mnyamaze ili mupate kurehemiwa". (Al
AƔraaf: 204).
Wamesema
wengi wa wafasiri wa Qur'ani kwamba Aya hii imeteremshwa kukhusu khutba ya Sala
ya Ijumaa. Na imeitwa hii khutba kwa jina la Qur'ani kwa vile imo ndani yake
Qur'ani Tukufu. Na qauli ya Mtume s.a.w.:
" Ukisema kumwambia sahibu yako
kwenye Sala ya Ijumaa na Imam anakhutubu - sikiliza - basi itakuwa umefanya
kosa". (Imehadithiwa na wapokezi wa Hadithi isipokuwa Ibni Maajah).
Na
rai nyengine ya Imam Shafi'ii r.a. ni kwamba haiharimishwi kusema, bali kusikiliza
ni sunna kama walivyopokea Al Sheikhan kuwa Sayyidna 'Uthman r.a aliingia
msikitini siku ya Ijumaa na Sayyidna 'Umar r.a. anakhutubia, akasema Sayyidna
'Umar r.a. kumwambia Sayyidna 'Uthman r.a.: "Nini hali ya watu
wanataakhari kuitikia wito?” Akasema Sayyidna 'Uthaman r.a.: “Yaa
Amir-l-Muuminiin! Baada ya kusikia adhana, nimetia udhu na nikaja
msikitini". Na imehadithiwa kuwa wakati Mtume s.a.w. yuko juu ya membari
anakhutubia siku ya Ijumaa aliingia mtu na kuuliza kwa kelele: "Lini
Qiyama"? Watu wakamuashiria anyamaze, lakini hakufanya hivyo. Na akarejea
na maneno yake, baada ya dakika Mtume s.a.w. akasema kumwambia: "Na uwe
pole, umekiandalia nini?” Akasema yule mtu: "Mapenzi ya
Mwenyezi Mungu na Mtume wake". Akasema s.a.w.: "Hakika yako wewe na
unaempenda". ( Imehadithiwa na Al Bayhaqy ).
Hoja
ya kwamba kusema wakati wa khutba si haraam ni vile kuwa Sayyidna 'Uthman r.a.
alisema kwa kumjibu Sayyidna 'Umar r.a., na kwamba Mtume s.a.w. hakumkanya yule
alieuliza lini Qiyama, na lau kama ni haraam basi angalimkanya kusema. Hii
khilafu iliopo kukhusu kusema au kutosema haikhusiani na kitu muhim na cha
dharura, katika hali hio haikatazwi kusema; bali ni waajibu kusema; kama vile
kumuongoza kipofu, au kuona mtu anatambaliwa na nnge ukamzindua, au kumuona dhaalim
amemuandama mtu ukamtanabahisha, au kuamrisha mema na kukataza maovu.
Wamekhitalifiana
rai wanazuoni juu ya kwamba mtu akiingia msikitini siku ya Ijumaa na Imam
anakhutubu, inajuzu asali raka'a mbili za tahiyatu-l-masjid au asisali.
Wamesema baadhi ya wanazuoni kuwa asisali, na imepokewa hivi kutoka kwa Ibni
'Umar r.a., na Sayyidna 'Uthman r.a. na Sayyidna 'Ali r.a.; na kwa hii amri ya
kusikiliza. Wakatoa dalili juu ya kisa cha Saliik r.a. kwamba alikuwa hana
nguo, Mtume s.a.w. akamuamrisha asimame ili watu wamuone wampe
sadaqa. Amesema Imam Shafi'ii r.a. na Ahmad na Is-haaq na wanazuoni wakisasa
wengine kuwa inapendekezwa asali tahiyatu-lmasjid raka'a mbili fupi kabla ya
kukaa, wao wametolea hoja hivi kwa qauli ya Mtume s.a.w. juu ya Saliik wakati
alipoingia msikitini akakaa kitako na Mtume s.a.w. anakhutubia kwenye Sala ya Ijumaa,
Mtume s.a.w. alimuuliza Saliik: "Umesali ewe fulani?”
Akajibu: "Laa", yaani si kusali; Mtume s.a.w.
akamwambia: ,
yaani inuka uruku'i, yaani usali. Na katika upokezi mwengine: yaani
inuka usali raka'a mbili. Na katika upokezi mwengine: yaani
sali raka'a mbili. Na katika upokezi mwengine:
"Akiingia
mmoja wenu msikitini siku ya Ijumaa na Imam anakhutubu, basi naasali raka'a
mbili". Na katika upokezi mwengine:
"" "…….,
na Imam anakhutubia, naaruku'i raka'a mbili, na azifupishe".
Hadithi
zote hizi zimo kwenye Kitabu cha Hadithi cha Imam Muslim r.a. na zimetaja wazi
kupendeza kusali raka'a mbili khafifu za (kuamkia
msikiti) unapoingia msikitini siku ya Ijumaa na Imam anakhutubu. Hivi ni kwa
mwenye kuingia msikitini na Imam ana khutubu. Ama yule aliyomo msikitini tangu
kabla ya Imam kuanza khutba, na akainuka kusali wakati Imam anakhutubu, hivi
haijuzu; hata ikiwa kwa raka'a khafifu.
Inasuniwa
kusoma Surat Al-Kahfi, usiku wa kuamkia Ijumaa (Alkhamis usiku kuamkia Ijumaa),
au Ijumaa yenyewe. Kusoma Surat Al-Kahfi mchana wa Ijumaa kumekuja kwa qauli ya
Mtume s.a.w:
"Mwenye
kusoma Surat Al-Kahfi siku ya Ijumaa hun'garishiwa nuru baina ya Ijumaa na
Ijumaa". (Imehadithiwa na Al Haakim na Al Bayhaqy).
Kusoma
Surat Al-Kahfi usiku wa kuamkia Ijumaa kumekuja kwa qauli ya Mtume s.a.w:
"Mwenye
kuisoma (yaani Surat Al-Kahfi) usiku wa kuamkia Ijumaa hun'garishiwa nuru
(yenye kuenea) baina yake na baina ya Bait-l-'atiiq (Msikiti wa Makka)".
(Imehadithiwa na Al Bayhaqy).
Ni
waajibu mtu anaposoma Qur'ani - Surat Al-Kahfi - au Sura nyengine yoyote ile,
iwe si kwa kumghasi au kumshawishi mwenzake anaesoma, au anaesali au mwenye
kuvuta uradi; kwa vile yeye kusoma kwa sauti ya kughasi. Kufanya hivyo ni
haraam, amesema Mtume s.a.w. :
"Hakika
kila mmoja wenu ni mwenye kusema na Mola wake Mlezi, basi musiudhiane, walaa
asitoe sauti mmoja wenu wakati akisoma". Wakati bora wa kusoma Surat
Al-Kahfi ni baada ya Sala ya alfajiri, kwa kukimbilia kheri. Ama vile
wanavyofanya watu wengi, yaani kuisoma msikitini na kwa sauti ya kughasi
wengine katika ibada zao, hivi haifai; bali imeharimishwa.
MAREJEO