Jumanne, 2 Oktoba 2018

HATA MIMI HUNIWEZI

HATA MIMI HUNIWEZI

Komeka adabu shika, zako jeuri zikome,
Jina unalo tajika, sikudanganye ndo ngome,
Yako ropoka ropoka, itakuja ikuchome,
Kama wale mewashindwa, hata mimi huniwezi,

Unenapo ukicheka, nanyakati uzisome,
Yasije kuja kufika, kutwa kuchwa ulalame,
Kwangu mekupa mkeka, sofani usiegeme,
Kama wale mewashindwa, hata mimi huniwezi,

Yanini yako mashaka, hali wajita kidume,
Roho kukupaparika, uenuke uiname,
Kwakijasho kukutoka, namihemo uiheme?
Kama wale mewashindwa, hata mimi huniwezi,

Chafua sita chafuka, kwako wazi niliseme,
Najua wakasirika, acha cheche niziteme,
Uvimbe nakuumuka, mithili ya paka shume,
Kama wale mewashindwa, hata mimi huniwezi,

Husuda zime kushika, wachoma kama umeme,
Kila kona wasifika, kwamajungu usipime,
Hupitwi na lakuzuka, liwe tanga liwe same,
Kama wale mewashindwa, hata mimi huniwezi,

Kwauzushi unanuka, hebu ndugu jitazame,
Wendako tadhalilika, kubali usikorome,
Watu tumesha kuchoka, anga hizi uzihame,
Kama wale mewashindwa, hata mimi huniwezi,

Wende wapi huna chaka, mwendo checheme checheme,
Ukiguswa unaruka, mwili teteme teteme,
Huwezi tena toroka, kila kona niukame,
Kama wale mewashindwa, hata mimi huniwezi,

Mtunzi:HD.Hassan
@SUKARI YA MASHAIRI@
Wete. Pemba
23/09/2018
02:21 asubuhi